Siasa

BoT kitendawili kigumu

WAKATI utata wa kujiuzulu kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Daudi Balali ukiendelea kutanda, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amepokea ripoti ya mwisho ya uchunguzi wa ubadhirifu ndani ya benki hiyo uliofanywa na Kampuni ya Ennst & Young.

Na Mwandishi Wa Majira


WAKATI utata wa kujiuzulu kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Daudi Balali ukiendelea kutanda, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amepokea ripoti ya mwisho ya uchunguzi wa ubadhirifu ndani ya benki hiyo uliofanywa na Kampuni ya Ennst & Young.


Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na kusainiwa na CAG, Bw. Ludovic Utouh, ilieleza kwamba ripoti hiyo imepokelewa baada ya rasimu ya awali ya uchunguzi huo kupokelewa Novemba 27 mwaka huu.


“Kama ilivyoelezwa kwenye taarifa hiyo, ripoti iliyopokelewa ilikuwa ni ripoti ya awali ambayo ilifanyiwa kazi na ofisi yangu na kurudishwa kwa wataalamu walioifanya kazi hii ili kukamilisha ripoti hii. Huu ni utaratibu wa kawaida wa kufanya kazi za ukaguzi hasa ikichukuliwa maanani kuwa Kampuni ya Ernst & Young, imefanya kazi hii kwa niaba yangu,” alisema Bw, Utouh.


Katika taarifa hiyo, Bw. Utouh, alisema mbali na uchunguzi wa ‘EPA Account’ya Benki ya Tanzania, hadidu za rejea za kazi hiyo ziliwataka wachunguzi kurejea ukaguzi wa hesabu za BoT za mwaka 2005/06, kazi iliyofanywa na Kampuni ya Hesabu ya TAC Associates ikishirikiana na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.


Alisema wachunguzi hao wametakiwa kutoa ripoti mbili tofauti moja ikiwa ni ya ‘EPA Account’ na nyingine ikihusu rejea ya ukaguzi wa hesabu za BoT kwa hesabu za mwaka 2005/06.


” Hivyo basi, napenda kutoa taarifa rasmi kwa Watanzania wenzangu ya kuwa nimepokea kutoka Kampuni ya Ernst & Young taarifa za mwisho za uchunguzi, siku ya Jumapili Desemba 23 (jana ). Kwa sasa nazipitia ripoti hizi mbili ili kujihakikishia usahihi wa yaliyomo kabla ya kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete katika juma la kwanza la Januari, 2008 baada ya kumaliza likizo yake, alisema Bw. Utouh.


Bw. Utouh amewahakikishia baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambao hivi karibuni walinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari wakieleza wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa taarifa ya uchunguzi huo, kuvurugwa na ofisi yake.


Bw. Utouh, alisema ripoti hiyo haijaandaliwa kwa maksudi kama inavyodhaniwa na kutokana na umuhimu wake kwa Taifa, ni lazima ifanyiwe kazi kwa umakini mkubwa na kuhakikisha mapendekezo yatakayotolewa, ni sahihi.


“Awali ya yote ripoti hii haijakaliwa kwa maksudi kama inavyodhaniwa. Ripoti hii ni muhimu sana kwa Taifa hivyo ni lazima ifanyiwe kazi kwa umakini mkubwa na kuhakikisha mapendekezo yatolewayo ni sahihi,” alisema.


Aliwahakikishia viongozi hao na Watzania kwa ujumla kuwa kamwe ripoti hiyo haiwezi kuvurugwa na kwamba Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ina uhuru kamili kwa kufuata sheria, kanuni na viwango vya taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu vya kimataifa.


Mbali na hilo alisema uchunguzi huo umefanywa na Enrst & Young inayotumia wataalamu kutoka nchi mbalimbali duniani zikiwemo Uingereza, Afrika Kusini, Japan, Kenya na Tanzania na kuongeza kuwa uchunguzi huo umefanyika kitaalamu kwa kuzingatia taratibu na viwango vya ukaguzi wa hesabu vya kimataifa.


Ameahidi kuwasilisha ripoti hizo kwa Rais Kikwete kama zilivyokabidhiwa kwake na wachunguzi wa suala hilo.


Sambamba na uchunguzi huo,vyombo vya habari wiki iliyopita viliripoti taarifa ya kujiuzulu Gavana wa BoT, Bw. Balali.


Gavana Balali anadaiwa kuomba kujiuzulu wadhifa huo kutokana na matatizo ya kiafya ambapo amelazwa kwa miezi mitatu baada ya kufanyiwa operesheni kubwa, Boston nchini Marekani.


Pamoja na taarifa za kujiuzulu kwake,kupitia barua yake iliyosambazwa kwa vyombo vya habari, Serikali kupitia Waziri wa Fedha Bibi Zakhia Meghji, wiki iliyopita, ilisema haina taarifa zozote za kujiuuzulu Bw. Balali zaidi ya kusoma jambo hilo magazeti.


Bibi Meghji, alisema hadi alipozungumza na waandishi, Ijumaa iliyopita, alikuwa hajapokea barua yoyote ya kujiuzulu Bw. Balali.


” Mimi ni Waziri wa Fedha sina taarifa hiyo, kwa kawaida katika ofisi yetu na hata nyingine mtu akitaka kuchukua hatua nyingine kuna utaratibu wa kuandikana barua. Mimi katika ofisi yangu sikuletewa na sina barua hiyo,” alisema Bibi Meghji.


Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu. Bw. Salvatory Rweyemamu naye alikaririwa akisema suala la kujiuzulu kwa Bw. Balali lilipaswa kuzungumziwa na Rais Kikwete lakini kwa sasa yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka.


Uchunguzi ndani ya BoT ulitokana na shinikizo kutoka kambi ya upinzani kupitia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Wilbrod Slaa baada ya kutangaza ilichokiita orodha ya mafisadi huku Bw. balali akituhumiwa kuhusika na ubadhirifu ndani ya benki hiyo.


Baada ya hapo Serikali iliagiza kufanyika uchunguzi ndani ya benki hiyo ili kubaini kama kulikuwa na ubadhirifu ndani ya BoT, hususan katika ujenzi wa majengo mawili pacha, ‘twin tower’ ya benki hiyo.



Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents