Siasa

BOT ndani ya kashfa nyingine

WAKATI bado ikiwa imegubikwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeingizwa katika tuhuma nyingine ya ulaji ambayo inahusisha posho za vikao vya wafanyakazi wake maarufu kama ‘105’.

Na Ramadhan Semtawa


WAKATI bado ikiwa imegubikwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeingizwa katika tuhuma nyingine ya ulaji ambayo inahusisha posho za vikao vya wafanyakazi wake maarufu kama ‘105’.


Hizi ni tuhuma mpya kuibuliwa ndani ya taasisi hiyo nyeti ya fedha nchini, ukiacha zile za ujenzi wa Majengo Pacha ( Twin Towers) na Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).


Habari kutoka ndani ya BoT, zinaeleza kuwa ulaji huo unatokana na posho hizo maarufu kama 105 ambazo kwa kila mfanyakazi anayehudhuria vikao vya ndani hulipwa Sh 105,000.


Hata hivyo, Naibu Gavana wa BoT (Utawala) Juma Reli, aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam hivi karibuni kwamba tuhuma za namna hiyo sisi chochote bali zinalenga kuichafua benki hiyo.


Reli ambaye hata hivyo, alikiri kuwepo kwa posho hizo maarufu kama ‘105’, alisema fedha hizo hulipwa katika vikao vya kujadili miradi.


Kwa mujibu wa Reli, si kweli kwamba watu wanalipana fedha hizo hata kama hawafanyi kazi ya maana.


“105 ni posho zinazolipwa wakati wa kujadili miradi, ni kweli zipo lakini hulipwa wakati wa vikao tu,” alisema Reli baada ya kuulizwa kuhusu kitu kinachoitwa 105.


“Siyo kweli kwamba watu wanajilipa tu bila kufanya kazi, hii ni posho ya kukaa wakati wa kujadili miradi,” alisisitiza Reli.


Alisema kila idara ina miradi yake ambayo wakati wa kujadiliwa, wahusika hupatiwa posho bila kujali kama inafanyika nje ya benki au ndani.


“Ni sawa na wewe, inatokea kazi kuhusu kujadili aua kuandika rasimu ya vyombo vya habari, si utapaswa kupewa posho kidogo ndiyo utaratibu tunaotumia hapa, hakuna namna nyingine,” alisisitiza Reli.


Hata hivyo, taarifa hizo kutoka kutoka BoT zinaeleza kwamba chini ya utaratibu huo wa ‘105’ watendaji wa idara na baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakijiingizia fedha kwa kuitisha vikao hata visivyokuwa vya msingi.


Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari kutoka BoT, utaratibu huo umekuwa ni kama mradi wa baadhi ya wakubwa ambao sasa unaonekana kushika kasi.


Vyanzo hivyo vya viliongeza kwamba, wakati mwingine baadhi ya wakuu wa idara huamua kuitisha kikao hata cha muda mfupi ili kujihalalilishia posho hiyo.


BoT ambayo ni mhimili mkuu wa mwelekeo wa uchumi wa nchi, katika miaka ya hivi karibuni imekumbwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi.


Tuhuma za ufisadi ndani ya EPA kwa sasa ndizo ambazo zimekuwa zikijadiliwa kufuatia kufanyika uchunguzi huru uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young, ambao matokeo yake yanasubiriwa kwa hamu.


Hata hivyo, ripoti hiyo imekuwa ikizidi kupigwa danadana ikielezwa kumsubiri Rais Jakaya Kikwete.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents