Burudani

Bozi Boziana Atua Bongo

Mwanamuziki nyota barani Afrika, Abubakar Benz almaarufu kama Bozi Boziana kutokea Congo DRC, aliwasili nchini jana mchana, maalumu kwa onyesho la aina yake lililopangwa kufanyika Novemba 28 kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni Dar es Salaam.

Msanii Bozi Boziana atafanya maonyesho kadhaa ambayo atapangiwa na uongozi wa bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ sambamba na kufyatua nyimbo za pamoja na mwanamuziki huyo.

 

Bozi Boziana aliwasili akiwa na msafara wa wanamuziki sita, ambapo akiwa Dar-Es-Salaam pamoja na msafara wake, watafanya mazoezi siku chache na baadaye ngoma yao itatambulishwa kwa wapenzi. Kwa wa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET), Asha Baraka, maonyesho hayo yamepangwa kufanyika Novemba 28 na mengine yatatangazwa baadaye.

Asha alisema, hatua ya Twanga Pepeta kufanya onyesho na Bozi Boziana ambaye ni mkongwe katika muziki wa dansi barani Afrika na nje, ni sehemu ya mpango wao kujitangaza katika soko la kimataifa.

Alisema kuwa mara baada ya maonyesho hayo, wanamuziki wengine wa Bozi Boziana wataondoka nchini na mkongwe huyo kubaki, akiandaa albamu mpya ambayo atairekodi akiwa na wanamuziki wa Twanga. Aliongezea kuwa albamu hiyo itakuwa na lugha mchanganyiko ya Kilingala na Kiswahili na baada ya kukamilika utunzi wake, itakwenda kufanyiwa ‘mixing’ nchini Ufaransa.

“Bozi Boziana ataimba Kilingala na baadhi ya maneno kuimba Kiswahili, wanamuziki wetu wataimba Kiswahili na Boziana kuimba ubeti huo huo Kilingala, lengo hapa ni kupromoti lugha yetu kwani naamini albamu hii itauza DR- Congo na nchi nyinginezo,” alisema Asha maarufu kama Iron Lady.

Asha, amewaomba wadhamini mbalimbali kujitokeza kusaidia kufanikisha maonyesho hayo na maandalizi ya albamu hiyo.

Alifafanua kuwa bendi yake pia itaendelea na maandalizi ya albamu mpya, ambapo hadi sasa wamekwishakamilisha nyimbo nne.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents