Bongo5 Exclusives

Breaking: Taarifa ya IGP Mwema kuhusiana na mauaji ya kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Liberatus Barlow

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishina Msaidizi wa Polisi Liberatus Barlow

Kufuatia mauaji ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, ACP, Liberatus Barlow, Inspekta Jenerali wa Polisi, Said A. Mwema ametoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo kama ifuatavyo:

1. Ndugu wananchi. Napenda kutumia fursa hii kuwapa taarifa kuhusu tukio la mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishina Msaidizi wa Polisi Liberatus Barlow yaliyofanywa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia leo tarehe 13/10/2012 majira ya saa saba usiku Mkoani Mwanza.

2. Tukio hilo limetokea wakati kamanda huyo akitokea kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake eneo la Frolida hotel Mwanza mjini, akiwa na ndugu yake waliyeongozana nae kutoka kwenye kikao hicho. Wakati akimshusha huyo ndugu yake eneo la Kitangiri Minazi Mitatu, walitokea watu wanaosadikika kuwa ni majambazi, na kumvamia na kuanza kumshambulia kwa risasi na kumuua papohapo.

3. Ndugu wananchi, kufuatia tukio hilo, tayari nimemtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI Robert Manumba kwenda mkoani Mwanza kwa lengo la kuimarisha ulinzi na upepelezi wa tukio hilo.

4. Najua tukio hili limetushitua na kutuhuzunisha wote. Hivyo, wakati tukiendelea na taratibu zingine kuhusiana na tukio hilo, niwaombe wananchi wote kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, utakaowezesha kuwabaini wahalifu hao.

5. Tutaendelea kuwapa taarifa za tukio hilo, kadri tutakavyoendelea kuzipata.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents