Habari

Buffalo wapangaji wa Trafiki Moshi

KUNA madai kuwa madereva wa mabasi ya Buffalo wamejenga kiburi na kuendelea kuendesha mabasi hayo kwa mwendo kasi kutokana na uhusiano wa karibu uliopo kati ya kampuni hiyo na Jeshi la Polisi.

Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam


KUNA madai kuwa madereva wa mabasi ya Buffalo wamejenga kiburi na kuendelea kuendesha mabasi hayo kwa mwendo kasi kutokana na uhusiano wa karibu uliopo kati ya kampuni hiyo na Jeshi la Polisi.


Madai hayo yanaongezewa nguvu na ukweli kuwa hata kituo cha mabasi hayo katika mji wa Moshi kipo eneo la kikosi cha Usalama barabarani mkoa wa Kilimanjaro hali inayojenga hisia kuwa wamekuwa wakibebwa.


Vyanzo mbalimbali vimelidokeza Mwananchi Jijini Dar es Salaam na Moshi kuwa sehemu ya fedha zilizotumika kujenga jengo la makao makuu ya Trafiki mkoani Kilimanjaro zina uhusiano na mapato ya kampuni hiyo.


Kampuni hiyo ya mabasi ya Buffalo ndiyo inayoendesha baa na hoteli ya Trafiki mjini Moshi ambayo sasa inatumika pia kama kituo cha mabasi ya Buffalo.


Habari za uhakika kabisa kutoka ndani ya makao makuu ya Jeshi la polisi zimedokeza kuwa mmiliki huyo wa Buffalo alikodishiwa eneo hilo na polisi kwa kodi ya Sh500, 000 kwa mwezi.


Sehemu ya fedha hizo ndizo zilizotumika kuendeleza ujenzi wa Jengo la makao makuu ya Trafiki mkoa Kilimanjaro na inadaiwa kuwa mkataba huo ulisimamiwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo (jina linahifadhiwa kwa sasa).


Baadaye wafadhili mbalimbali walijitokeza baada ya kuhamasishwa na kamanda huyo ambapo baada ya kukamilika lilifunguliwa rasmi na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.


Imeelezwa, hata eneo ilipojengwa baa hiyo halikuwa mali ya polisi bali lilikuwa ni la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na kwamba kwa mujibu wa ramani, eneo la trafiki linaishia pale lilipo jengo la makao makuu ya Trafiki Kilimanjaro.


Mwishoni mwa mwa 1998, suala la polisi kupora eneo hilo na kuruhusu kujengwa kwa Baa hiyo kuliwahi kuibua mvutano mkubwa kati ya polisi na Halmashauri lakini inadaiwa polisi walitumia ubabe kuzima mvutano huo.


Meya wa Manispaa ya Moshi wakati huo, Denis Chuwa aliwahi hata kulalamika waziwazi kuwa Halmashauri yake ilizuiwa ilipokwenda eneo hilo kubandika notisi ya kutaka jengo hilo libomolewe.


Mbali na mabasi ya Buffalo kutumia baa na hoteli hiyo kama kituo chao cha mabasi lakini inadaiwa baa hiyo imekuwa ni ‘kijiwe’ cha askari Trafiki kwa kuwa kuna vyumba maalumu vya siri ambavyo huvitumia kwa masuala binafsi.


Polisi mmoja ambaye alidai anafahamu vyema suala hilo, aliliambia Mwananchi kuwa baadhi ya mabasi ya Buffalo yamekuwa yakiendeshwa kwa mwendo kasi kiasi cha kupewa jina la Mnyama.


Miaka ya nyuma wakati Yusuph Makamba akiwa mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani aliwahi kumkemea waziwazi mmiliki huyo kwamba pamoja na utajiri wake lakini alikuwa ameajiri baadhi ya madereva vichaa.


Makamba ambaye alikuwa akizungumza na wamiliki wa mabasi, alitoa mfano kuwa wakati anatoka Dar kuja Moshi akiwa katika mwendo wa kilometa 140, alipitwa na basi moja la Buffalo kana kwamba gari lake lilikuwa limesimama.


Lakini pamoja na ukali huo wa Makamba bado baadhi ya madereva wa mabasi hayo hawakubadilika kiasi kwamba wananchi wamejawa na hisia kuwa huenda magari hayo yana mkono wa vigogo.


Wananchi mbalimbali waliohojiwa wadai kuwa ili Jeshi la polisi lionekane halibebi kampuni hiyo basi halina budi kuvunja ndoa baina yao ili kuondoa kuwepo kwa mgongano wa maslahi katika utendaji.


Naye Hussein Issa anaripoti kuwa baada ya uongozi wa mabasi ya Buffalo kufunga ofisi zake ili kutoa fursa kwa kushiriki kikamilifu katika maombolezi, nauli za kwenda Arusha na Kilimanjaro zimepanda.


Katika uchunguzi uliofanywa na Mwananchi jana ulibaini kuwa kutokana na mabasi kuwa machache sasa nauli ni kuanzia shilingi 16,000 na 18,000.


“Tunateseka kweli yaani hii ajali imetufanya tushindwe kabisa kusafiri kwani kila gari ukiligusa nauli bei juu. Sasa ni shilingi 18,000 imetokea wapi tena wakati tunajua nauli ni kuanzia 10,000 mpaka 12,000”alisema John Moshi ambaye alikuwa anataka kwenda Moshi.


Mwananchi ilipofika katika ofisi za basi hilo katika kituo cha mabasi cha Ubungo jana ilikuta ofisi hiyo imefungwa kwa madai kwamba wahusika wanashiriki maombolezo.


“Ofisi zimefungwa kwani wewe hujui kuwa Buffalo imepata ajali, wameenda kuomboleza huko Moshi”alisema mpiga debe aliyejitambulisha kwa jina moja la Deo.


Kwa upande mama Hawa ambaye ni abiria akiwa katika gari la Saibaba alisema kinachoumiza ni kuwa nauli zimepanda hadi Sh 18,000. Kampuni ya Buffalo inamiliki zaidi ya mabasi 10 yanayofanya safari zake Dar es Salaam, Moshi na Arusha.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents