Habari

Bunge hatuna rekodi ya Mh. Nyalandu kujiuzulu ubunge – Spika Ndugai

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesisitiza kuwa bado hajapata barua ya kujiuzulu nafasi ya ubunge katika Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu haijafika ofisini kwake, hivyo anamtambua kiongozi huyo kuwa bado ni mbunge.

Ndugai aliyasema hayo jana alipozungumza kwa njia ya simu na gazeti la Habarileo, kuhusu kama ofisi yake imeipata barua hiyo na hatua zinazochukuliwa baada ya mbunge huyo kujiuzulu ubunge na kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Yaani haya mambo mie ninayasikia kwenu tu (waandishi wa habari) na kwenye vyombo vya habari. Sisi kama Bunge mpaka sasa hatuna rekodi yoyote ya Mheshimiwa Nyalandu kujiuzulu nafasi yake ya ubunge,” alisisitiza Ndugai.

“Kwa maana rasmi mpaka sasa (jana mchana) mimi kama Spika sitambui kujiuzulu kwa Nyalandu, na ninamtambua kuwa bado ni mbunge wa Singida Kaskazini, na hata akija katika Bunge lijalo, nitampokea kwa mikono miwili hadi pale nitakapopata rasmi barua yake,” alisisitiza.

Mh. Nyalandu juzi alitangaza mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha, kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama ya CCM ikiwemo ujumbe wa Halmashauri Kuu na kukiomba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumpokea kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa hali ya siasa nchini.

Hata hivyo Mh. Nyalandu alisema tayari amemwandikia Spika wa Bunge Ndugai, barua ya kujiuzulu nafasi yake ya ubunge aliyoitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu alipochaguliwa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents