Burhan kiongozi mpya Sudan, Waziri mkuu kuapishwa baadaye
Kiongozi wa jeshi Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan ameapishwa kuwa kiongozi mpya wa Sudan.
Wanachama wa Baraza jipya tawala, ambalo litaongozwa na Burhan, pia wameapishwa katika mji mkuu Khartoum.
Hafla hiyo imefanyika saa chache baada ya Baraza la Mpito la Kijeshi na vuguvugu la upinzani linalopigania demokrasia nchini humo kuunda baraza tawala lenye wanachama 11 wakiwemo wawakilishi wa kijeshi na kiraia, kuiongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu kuelekea katika utawala wa kiraia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la DW, Burhan ataongoza baraza hilo lenye raia sita na maafisa watano wa kijeshi, kwa miezi 21 ijayo.
Raia atachukua usukani kutoka kwa Burhan kumalizia miezi 18 itakayosalia hadi 2022 wakati uchaguzi utakapoandaliwa.
Waziri Mkuu anatarajiwa kuapishwa baadaye leo.
Nafasi hiyo inatarajiwa kuchukuliwa na mchumi Abdalla Hamdok, ambaye alihudumu kama waziri wa fedha katika miaka ya 80.