Siasa

Bush kuwasili leo, kusaini mkataba mkubwa

RAIS George Bush wa Marekani anawasili nchini leo na kesho atasaini mkataba mkubwa wa dola za Marekani milioni 698 chini ya mpango wa Changamoto za Milenia (MCC), ambao haujawahi kusainiwa nchini.

Na Waandishi Wa Majira

 

 

 

RAIS George Bush wa Marekani anawasili nchini leo na kesho atasaini mkataba mkubwa wa dola za Marekani milioni 698 chini ya mpango wa Changamoto za Milenia (MCC), ambao haujawahi kusainiwa nchini.

 

 

 

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Bw. Salvatory Rweyemamu, alisema Rais Bush atamaliza ziara yake nchini Jumanne ijayo.

 

 

 

Alisema Rais Bush atafuatana na mkewe, Mama Laura, wakitokea Benin. Wengine katika msafara wake ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bibi Condeleeza Rice na ujumbe mkubwa, wakiwamo waandishi wa habari zaidi ya 170.

 

 

 

Akifafanua kuhusu matumizi ya fedha hizo, Bw. Rweyemamu alisema zimelenga kusaidia miradi ya afya, miundombinu na umeme mkoani Kigoma.

 

 

 

Alisema fedha hizo zitatumika kujenga barabara tatu muhimu ambazo ni Horohoro mpaka Tanga, Tunduru, Songea hadi Mbambabay na Tunduma hadi Sumbawanga.

 

 

 

Alisema ziara hiyo ni muhimu kwa Tanzania, kwani itanufaisha sehemu nyingi na ni mara ya kwanza kwa Rais wa Marekani kukaa muda mrefu katika nchi za Afrika jambo ambalo ni heshima kubwa kwa Tanzania.

 

 

 

Bw. Rweyemamu alisema baada ya Rais Bush kusaini mkataba huo, mchana atatembelea hospitali ya Amana na Jumatatu atakwenda Arusha.

 

 

 

Wakati huo huo, Mama Laura anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mpango wa Kazi wa watoto Yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi unaosimamiwa na Mama Salma Kikwete.

 

 

 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Bw. Alfred Tibaigana, alisema katika ziara hiyo, barabara zitakazofungwa ni Nyerere, Pugu, Gerezani na Sokoine ambayo itafungwa leo alasiri.

 

 

 

Nyingine ni Sokoine, Luthuli, Ocean, Kivukoni, Gerezani, Nyerere hadi makutano ya Kawawa, Uhuru hadi Old Bagamoyo zitafungwa asubuhi kesho na Barabara za Ali Hassan Mwinyi, Ocean, Luthuli na Sokoine zitafungwa mchana.

 

 

 

Alisema Jumatatu barabara za Sokoine, Ohio, Kivukoni, Gerezani, Nyerere hadi makutano ya Pugu zitafungwa kuanzia asubuhi na jioni.

 

 

 

Naye Eben-Ezery Mende anaripoti kuwa Waislamu Dar es Salaam, jana waliandamana kupinga ujio wa Rais Bush kwa walichodai kuwa kuja kwake kuna lengo la kuandaa mazingira ya kuteka raslimali za nchi.

 

 

 

Akizungumza Dar es Salaam jana kabla ya maandamano hayo kuanza, Mwenyekiti wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, alidai kuwa Waislamu wote nchini wanapinga ujio huo na kuamini kuwa kuja kwa Rais Bush kutaiweka nchi katika hali ya hatari kwa siku chache zijazo.

 

 

 

“Kunyamaza ni dhahabu na kuzungumza ni fedha. Hivyo tunaamini kuwa Bush anakuja nchini kesho (leo) ila tumeona tumpokee kwa mabango yanayomwonesha kuwa anafahamika kuwa ni kiongozi asiyefaa na anayetawala kibeberu,” alisema Shekhe Ponda.

 

 

 

Alisema tetesi zilizopo katika ujio huo ni kuwa ana mpango wa kutafuta makoloni kwa kuiteka nchi kisiasa na kuweka kambi yake ya kijeshi na kubainisha kuwa utaratibu huo unafanywa na Rais huyo kwa nchi zilizokosa uzalendo wa raslimali zao.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents