Habari

Bwana harusi afa kwa homa bonde la ufa

BWANA harusi aliyekuwa kwenye fungate mkoani Arusha amekufa kwa homa ya bonde la ufa na kufanya idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo hadi sasa kufikia watano, kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Paul Sarwatt, Arusha

 

BWANA harusi aliyekuwa kwenye fungate mkoani Arusha amekufa kwa homa ya bonde la ufa na kufanya idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo hadi sasa kufikia watano, kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

 

Bwana harusi huyo ametajwa kuwa ni Kisioki Kipong’i (25) mkazi wa kijiji cha Lesmangori wilayani Monduli ambaye alizikwa chini ya usimamizi mkali wa wataalamu wa afya wa wilaya hiyo Februari 21 mwaka huu.

 

Akizungumza jana, mmoja wa maofisa wa serikali wilayani Monduli ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema Kipong’i ambaye alikuwa mfanyakazi wa shirika moja mjini Arusha alikumbwa na mauti baada ya kwenda kijijini kwao kuoa.

 

“Kipong’i alifunga ndoa Februari 11 mwaka huu kwa ndoa ya mila za Kimasai na alikuwa kwenye fungate kijijini kwao kabla ya kurudi kazini kwake mjini Arusha,” alisema. Ofisa huyo wa afya alisema wakati akiwa katika fungate hiyo, ng’ombe mmoja katika familia yao alikufa ghafla, wakati wakimchuna ngozi, ndipo Kipong’i alipoambukizwa kwa kushika damu ya mnyama huyo.

 

“Wanafamilia walikuwa wamechukua tahadhari ya kutokula nyama ya ng’ombe huyo na waliamua kumchuna wapate ngozi lakini hawakutumia vifaa vya kujikinga wakati wanamchuna,” alisema. Alisema baada ya siku mbili Kipong’i alianza kujisikia vibaya na alipelekwa katika hospitali ya wilaya Monduli kwa matibabu ambako alikufa baada ya siku sita huku akivuja damu sehemu mbalimbali za mwili.

 

Mtaalamu huyo alisema dalili zote za mgonjwa huyo zilikuwa zinaonyesha kuwa alikuwa na virusi vya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa na tayari taarifa za kitaalamu zimepelekwa kwa ofisa afya mkoa wa Arusha.

 

Ofisa wa Afya Mkoa, Crispin Shayo alithibitisha kupokea taarifa za awali za kifo cha mgonjwa huyo lakini ofisi yake ilikuwa inasubiri taarifa za maandishi ili zifanyiwe kazi.

 

“Ni kweli maofisa wa wilaya wametueleza taarifa za kifo hicho lakini tunasubiri taarifa ya maandishi ambayo ninatarajia kuipata Jumatatu ili tuifanyie kazi,” alisema.

 

Dk. Shayo alisema kwa sasa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo wakati serikali ikijiandaa kutoa chanjo kwa mifugo yote mkoani Arusha.

 

Ugonjwa huo hatari ambao kwa mara ya kwanza uliripotiwa kuingia mkoani hapa Januari 31 umeleta athari kubwa za uchumi na jamii kwa wananchi. Pamoja na kuvurugika kwa biashara ya nyama, bei ya vitoweo vingine kama samaki na kuku vimepanda bei maradufu.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents