Siasa

CCM yafanya maamuzi mengine mazito

KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imefanya maamuzi mengine mazito yakiwemo kuridhia kuwatimua madiwani watano wa chama hicho, kusimamisha viongozi wawili zaidi wa Jumuiya ya Wazazi

Na Theodatus Muchunguzi, Dodoma


KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imefanya maamuzi mengine mazito yakiwemo kuridhia kuwatimua madiwani watano wa chama hicho, kusimamisha viongozi wawili zaidi wa Jumuiya ya Wazazi, maafisa wengine wa chama kutoka ofisi ndogo Lumumba jijini Dar es Salaam na Makao Makuu Dodoma.


Pia CC kimemuengua mgombea mmoja wa uenyekiti wa CCM wa Mkoa.


Kamati Kuu katika kikao chake kilichofanyika kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu, imetangaza kumvua haki ya kuchaguliwa katika uongozi wa CCM, Thomas Nyimbo, baada ya kuthibitika kuwa tabia na mwenendo wake vinamfanya asistahili kuwa na haki hiyo.


Nyimbo alikuwa ni mmoja wa wagombea wa kiti cha uenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, akichuana na wagombea wengine, akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Japhet Mangula. Hivi karibuni Nyimbo amekuwa akitoa shutuma nyingi dhidi ya mgombea mwenzake, Mangula.


Taarifa iliyotolewa mjini hapa jana mchana na kusainiwa na Katibu wa Halmashauri ya Kuu ya Taifa wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Aggrey Mwanri, ilieleza kuwa Kamati Kuu imechukua hatua ya kumpa adhabu hiyo kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili, toleo la 2002, kifungu cha 8.2.4.


“Hatua hiyo imezingatia ukweli kuwa Nyimbo aliwahi kupewa adhabu ya karipio kwa tabia na mwenendo huo huo, lakini amerudia tena,” ilieleza taarifa hiyo na kuongeza kuwa Nyimbo atatumikia adhabu hiyo kwa miezi 24 (yaani miaka miwili).


Chama hicho pia kilithibitisha taarifa zilizochapishwa na baadhi ya magazeti kuhusiana na kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abiuod Maregesi na Katibu Mkuu, Cosmas Hinju, kwa kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za jumuiya hiyo.


Hata hivyo, katika taarifa hiyo, CCM iliongeza majina mawili ya Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Ramadhan Suleiman Nzori na Babilas Mpemba miongoni mwa viongozi waliosimamishwa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi hao watatu wa kitaifa wa Jumuiya ya wazazi wamesimamishwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, toleo la Mei 2005, kifungu cha 110 (7) wakati Mpemba amesimamishwa kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa chama hicho na jumuiya zake.


Lengo la hatua hiyo ya Kamati Kuu kuwasimamisha ni kutoa nafasi kwa vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa tuhuma kabla ya uamuzi kamili juu yao kutolewa, ilieleza taarifa hiyo bila kuzungumzia chochote kuhusiana na tuhuma zinazowakabili, mbali na kusema kuwa walitumia vibaya madaraka yao.


Kamati Kuu haikuzungumzia chochote kuhusiana na taarifa za kufukuzwa kazi kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Mujuni Kataraiya kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za chama wakati alipokuwa Katibu wa chama hicho Mkoa wa Mwanza kabla ya kuhamishiwa Singida.


Kamati Kuu pia imeridhia uamuzi wa kuwafukuza uanachama madiwani watano kwa tiketi ya CCM wilayani Tunduru, kutokana na kukiuka maadili ya chama. Kamati hiyo iliyomaliza kikao chake juzi usiku chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Rais Jakaya Kikwete, imesema uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Ruvuma hivi karibuni wa kutoa adhabu ya kuwafukuza uanachama madiwani hao ulikuwa sahihi.


Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Ruvuma iliwafukuza uanachama madiwani hao baada ya kuthibitika kuwa wamekiuka maadili ya uongozi na ya uanachama. Taarifa ya Mwanri ilieleza kuwa walifukuzwa kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili toleo la Mei 2002 kifungu namba 8.2.9.


Miongoni mwa waliofukuzwa uanachama na hivyo kupoteza wadhifa wa udiwani walioupata kwa tiketi ya CCM ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Burhan Makonje. Wengine ni Zuhura Mafutari, Suleiman Shaibu Chisopa, Aindi Bakari Darwesh na Halima Hamis Luambano.


Taarifa ya CCM ilisema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, mtu anapokosa sifa ya uanachama wa chama cha siasa moja kwa moja anapoteza nafasi ya uongozi wa kuchaguliwa aliyoipata kupitia chama kinachohusika.


Madiwani hao waliofukuzwa waliitwa mjini hapa na kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM wiki iliyopita kuhusiana na tuhuma zilizokuwa zinawakabili. Waliongozana na baadhi ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya Tunduru, akiwemo Katibu wa chama hicho wa wilaya hiyo, Livingstone Lusinde. Hata hivyo, taarifa hiyo ya CCM haikueleza majina mengine ya vigogo ambao wameenguliwa.


Viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakikataa kuzungumza na waandishi wa habari kwa maelezo kuwa taarifa zozote kuhusiana na maamuzi zitakuwa zinatolewa baada ya vikao husika kumalizika Kamati Kuu pia imepitisha majina ya wagombea watatu wa nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha. Waliopitishwa ni Anaelson Ole Joel, Laurence Heddi na Julios Ole Sekayan. Uchaguzi huo utafanyika kujaza nafasi hiyo iliyoachwa wazi kutokana na kujiuzulu kwa Paulo Lotha Laizer.


Wakati huo huo, Kamati Kuu ilisema kuwa imepitia majina ya Wana-CCM walioomba uongozi ngazi ya wilaya, mkoa na taifa na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu iliyoanza kikao chake cha siku mbili jana, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuteua majina ya watakaogombea uongozi wa CCM katika ngazi hizo.


Habari kutoka ndani ya kikao cha NEC kinasema kwamba mvutano mkubwa ulitokea katika kikao cha Kamati Kuu, ambapo kundi kubwa la wazee lilikuwa limekatalia kabisa baadhi ya wenzao kuenguliwa.


Souce: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents