Siasa

CCM yataka mkutano na CUF mwezi huu

KATIBU Mkuu wa CCM, Bw. Yusufu Makamba, amemshauri Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, amtake Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Mazungumzo ya vyama hivyo upande wa CUF, aangalie uwezekano wa kukutana

Na Mwandishi Wa Majira


 


KATIBU Mkuu wa CCM, Bw. Yusufu Makamba, amemshauri Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, amtake Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Mazungumzo ya vyama hivyo upande wa CUF, aangalie uwezekano wa kukutana haraka mwezi huu.


Katika barua yake kwa Maalim Seif iliyoandikwa Aprili mosi mwaka huu, Bw. Makamba alisema upande wa CCM wako tayari kukutana na Kamati ya CUF ili kuwasilisha uamuzi wa maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM “kama tulivyokubaliana”.


Bw. Makamba katika barua hiyo, anaeleza mambo yaliyojadiliwa na NEC Butiama mkoani Mara, yaliyokubaliwa na yaliyohitaji marekebisho.


Mambo yaliyojitokeza katika mkutano wa Butiama Machi 29 na 30 mwaka huu kwa mujibu wa barua hiyo, ni mapendekezo yaliyokubaliwa na NEC bila marekebisho kama yalivyo katika rasimu ya makubaliano ya Kamati ya Mazungumzo.


Pia kuna mambo machache yaliyokataliwa yanayohusiana na utaratibu wa muundo wa Serikali shirikishi itakayoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.


Mengine ni mambo yaliyotolewa maelekezo maalumu na Halmashauri Kuu ya Taifa juu ya utaratibu ulioonekana unafaa zaidi wa kufikia lengo la kuundwa kwa Serikali shirikishi.


Barua ya Bw. Makamba imenakiliwa kwa Rais Jakaya Kikwete, Rais Amani Abeid Karume, Profesa Ibrahim Lipumba na wenyeviti wenza wa Kamati, Bw. Kingunge Ngombale-Mwiru(CCM) na Bw. Hamad Rashid Mohammed (CUF).


Nao Said Mwishehe na Benedict Kaguo wanaripoti kuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amesema lazima CCM na CUF waweke wazi mambo waliyokubaliana wakati wakitafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar ndipo wananchi watoe maoni yao.


Akizungumza Dar es Salaam jana na waandishi wa habari, Mchungaji Mtikila alisema anaunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kutaka uamuzi wa kujadili Serikali ya Mseto kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ufikiwe na wananchi kwa kutoa maoni yao kwanza.


Alisema suala muhimu kabla ya maoni ni masuala yaliyojadiliwa na viongozi wa vyama vyote viwili yawekwe wazi, ili wananchi wajue na hata wanapoanza kutoa maoni yao wafahamu kinachotolewa maoni.


Mbali ya kutaka masuala yaliyojadiliwa kuhusu muafaka yawe wazi, Mchungaji Mtikila alisema ipo haja ya wananchi kupewa elimu kwanza kuhusu Muafaka ndipo mambo mengi yafuate yakiwamo ya maoni.


Alisema wananchi wasipofahamishwa, kinachoendelea kuhusu masuala ya Muafaka na Serikali ya Mseto, itakuwa vigumu kutoa maoni ambayo mwisho wake yataleta maslahi kwa Watanzania wote.


“CCM ni watu wagumu sana linapofika suala la kushirikisha wananchi katika uamuzi mzito, lakini kwa hili wameanza kuonesha welewa, tunapaswa kuwaunga mkono. Sifurahishwi na viongozi wa CUF, kwani hawataki suala la Muafaka lijadiliwe na wananchi, wanaficha kitu gani hapa?,” alihoji Mchungaji Mtikila.


Akielezea hatua ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kwenda Jumuiya ya Kimataifa kuishitaki CCM kwa kuzorotesha mazungumzo ya Muafaka, Mchungaji Mtikila alisema haoni sababu ya kwenda huko wakati wao ndicho chanzo cha kukataa kuendelea mazungumzo kwa ya Muafaka kwa kushirikisha wananchi.


 


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents