Chenge azidi kuingia matatani

chenge_m.jpgKAMPUNI iliyokuwa ikimchunguza Waziri wa zamani wa Miundombinu, Adrew Chenge, imezidi kuja juu baada ya kuzibana kampuni nyingine ambazo zimekuwa…

 

KAMPUNI iliyokuwa ikimchunguza Waziri wa zamani wa Miundombinu, Adrew Chenge, imezidi kuja juu baada ya kuzibana kampuni nyingine ambazo zimekuwa zikiendesha shughuli zake kwa udanganyifu ili ziweze kujilimbikizia mabilioni ya vijisenti.

Katika kuhakikisha inawabana mafisadi juzi Kampuni hiyo ya SFO iliitoza Kampuni ya Severn Trent Water Ltd faini ya pauni milioni 2 (Sh Bilioni 4) kwa kutoa takwimu za uongo katika kanuni za uendeshaji wa makampuni ya maji nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kwenye tovuti ya SFO, kesi hiyo ilikuwa ikiunguruma katika Mahakama Kuu ya makosa ya jinai tangu mwanzoni mwa mwaka huu na faini iliyo ilitolewa baada ya kampuni hiyo ya Severn Trent Water (“STW”) kukiri makosa mawili ambayo yanakiuka sheria za viwanda vya maji ya mwaka 1991.

Mbali na kuitoza faini Kampuni hiyo pia Kampuni hiyo ya, Serious Fraud Office (SFO) ambayo inajihusisha uchunguzi wa makosa ya jinai kwa kushirikiana na polisi wa kituo cha Staffordshire, Polisi kutoka kituo cha Polisi cha Midlands Magharibi na Polisi wa kituo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza, waliendesha msako katika maeneo matano ya biashara ambao ni washirika wa kampuni ya Boston & Maine yaliyoko katika eneo la Staffordshire.

Majengo hayo matano yaliyokaguliwa katika eneo la Staffordshire, moja ni la biashara na mawili ni makazi binafsi, Birmingham, jengo binafsi wakati Manchester ukaguzi huo ulifanyika katika jengo la biashara.

Katika msako huo wanaume watatu na mwanamke mmoja walitiwa mbaroni ingawa waliachiliwa tena baadaye bila kufunguliwa mashitaka ila kwa dhamana ya Polisi.

Uchunguzi huo ambao ulianza tangu Februari mwaka huu ni kufuatia agizo kutoka idara ya Idara ya Biashara na Viwanda kuagiza uchunguzi ufanyike katika kampuni ya Boston & Maine na makampuni mengine ya aina hiyo ambayo yanatuhumiwa kununuliwa kwa njia ya udanganyifu.

Taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa shughuli za SFO zinawasumbua sana vigogo nchini ambao wako roho juu wakisubiri hatma ya uchunguzi dhidi ya Andrew Chenge na uchunguzi mwingine ambao huenda ukafanywa na taasisi hiyo kubaini vigogo zaidi waliojihusisha katika sakata la rada na kashfa nyingine zilizogubika nchi hii.

Gazeti moja maarufu la Uingereza liitwalo The Guardian mwanzoni mwa Aprili mwaka huu, lilichapisha habari na kuzisambaza kwenye mtandao wa intaneti likiweka wazi kwamba Chenge anachunguzwa kwa kuchimbia sh. bilioni moja kwenye akaunti yake iliyoko nje ya nchi anazodaiwa kuzipata kwa njia ya ufisadi.

Gazeti hilo lilisema kwamba taasisi moja makini ya kuchunguza makosa ya jinai nchini Uingereza ijulikanayo kwa kimombo kama Serious Fraud Office (SFO) inafanya uchunguzi ili kuona kama zinahusiana na zile zilizotolewa kwa njia ya rushwa katika ununuzi wa rada ya kijeshi.

SFO inachunguza tuhuma kwamba vigogo wa serikali ya Tanzania na wafanyabiashara kadhaa nje na ndani ya nchi, walikula njama kununua rada ya kijeshi kutoka Uingereza kwa sh. bilioni 70 mwaka 2002 kiasi ambacho ni karibu mara dufu ya bei yake halisi.

Katika dili hilo, inadaiwa kwamba kampuni ya BEA Systems ambayo ndio ilikuwa dalali katika biashara hiyo mbovu, ilitoa hongo ya jumla ya dola za Marekani bilioni 12 ili kuwapoza maafisa wa serikali wafanye juu chini kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanzania inanunua rada hiyo kwa bei mbaya.

Maafisa wa SFO walitinga nchini Aprili na kumpekua Chenge jijini Dar es Salaam na kisha kuhojiana naye kuhusu tuhuma hizo kabla ya kwenda Uingereza na kukuta amechimbia sh. bilioni moja kwenye akaunti yake. Chenge amekiri kwamba kweli pesa hizo ni zake.

Chenge mwenyewe aliporejea kutoka ziarani Ulaya wiki iliyopita alilalamika kwamba anasingiziwa na maadui zake kisiasa na kwamba hakupata pesa hiyo kwa ufisadi bali kwa mihangaiko yake mwenyewe na kwa maana hiyo asingeweza kujiuzulu kwa sababu tuhuma hizo zilikuwa bado zinachunguzwa.

Baada ya kubanwa na waandishi wa habari kuhusiana na tuhuma hizo, aliziita shilingi bilioni moja zilizokutwa kwenye akaunti yake katika akaunti binafsi nchini Uingereza kwamba ni vijisenti, lakini akaja kuomba radhi baadaye kwamba kwa lugha yao ya kisukuma neno vijisenti lina maana na pesa, iwe ndogo au nyingi.

Alijiuzulu baadaye na suala lake kuzua mjadala mzito kuhusu tuhuma za ufisadi zinazowahusisha moja kwa moja viongozi wa serikali wakiwamo wanasiasa wakongwe akiwemo Waziri Mkuu aliyejiuzulu pamoja na mawaziri wengine wawili mapema mwaka huu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents