Siasa

Chenge: Nimezushiwa

MBUNGE wa Bariadi Magharibi aliyejiuzulu uwaziri hivi karibuni kwa kashfa ya kukutwa na fedha zinazohusishwa na ufisadi, Andrew Chenge amewataka wananchi wa jimbo lake kuendelea kumwamini kwa kuwa yeye ni mtu safi

na Jane Kajoki, Bariadi




MBUNGE wa Bariadi Magharibi aliyejiuzulu uwaziri hivi karibuni kwa kashfa ya kukutwa na fedha zinazohusishwa na ufisadi, Andrew Chenge amewataka wananchi wa jimbo lake kuendelea kumwamini kwa kuwa yeye ni mtu safi na asiye na hatia yoyote kwani tuhuma dhidi yake ni za kuzushwa.

Mbali ya hilo, Chenge alisema alifikia uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wa Waziri wa Miundombinu zaidi ya wiki mbili zilizopita si kwa sababu ya kukiri makosa, bali ili kutoa fursa kwa taasisi zinazochunguza kashfa yake kufanya kazi yake kwa uwazi.

Chenge ambaye jana alihutubia mikutano ya hadhara katika maeneo ya Bariadi Mjini, Ramadi, Nyakabimbi na Kapiwi, alisema wakazi wa Dar es Salaam ndio ambao wamekuwa wakimuona kuwa mtu asiyefaa kutokana na kubebeshwa tuhuma zisizo za ukweli, ikiwa ni pamoja na kuzushiwa kifo.

“Dar es Salaam wanasema sifai labda kwa sababu ya sura yangu…Pamoja na watu wa Dar es Salaam kupiga kelele kuwa sifai, naamini sina hatia yoyote, na ndiyo maana nilijiuzulu. Ninyi wakazi wa jimboni kwangu ndio mnajua kama sifai au nafaa.

“Haya mambo yaliyotokea ni ajali ya kisiasa. Ni mambo ya kupikwa na watu, lakini kwa tuhuma hizi wacha tuwape nafasi waendelee na uchunguzi. Sitakiwi kuzungumzia hilo kwa sasa, nimekuja nyumbani kuhimiza shughuli za maendeleo katika jimbo letu katika nyanja zote za barabara, elimu, afya na maji,” alisema Chenge ambaye alivuta umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakimshangilia kila alipokuwa akihutubia.

Alisema pamoja na kujiuzulu uwaziri, aliahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa jimbo lake na akasema anaamini ifikapo mwaka 2010 atakuwa ametekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010.

“Walio na ndoto za ubunge tukutane kwenye hoja za utekelezaji wa ilani mwaka 2010. Mmeona tulivyojenga shule za sekondari, barabara, mabwawa, visima, vituo vya afya vyote hivyo ni katika jimbo letu. Pamoja na habari ya kuzushiwa kifo, nawaomba mtulie, tushirikiane kwa kutembea kifua mbele kufanya kazi na kujiletea maendeleo,” alisema Chenge ambaye anatembelea jimbo lake kwa mara ya kwanza tangu ajiuzulu.

Akiwa katika Kijiji cha Dutwa alisema alitaja vijisenti si kwa nia ya kukejeli bali akiwa na mtazamo wa Kisukuma ambao wao wanapoongelea ng’ombe 100 kwa mfano wanasema ‘vijing’ombe’.

Hii ni mara ya pili kwa Chenge kuzungumzia kauli yake ya vijisenti ambayo kwa kiwango kikubwa ndiyo inayoonekana kuwa iliyokuza tuhuma alizokuwa akihusishwa nazo.

Kwa mara ya kwanza, Chenge alizungumzia kauli yake hiyo jijini Dar es Salaam wakati alipofanya mahojiano kwa njia ya simu na gazeti hili, ambapo aliwaomba radhi Watanzania ambao walikwazika au kuumizwa na kauli yake hiyo ya vijisenti.

Alisema halikuwa lengo lake kuwakera wananchi kwa kauli hiyo iliyozua mjadala kiasi cha baadhi ya makundi ya watu wa kada tofauti kutoa maoni yao wakimtaka Rais Jakaya Kikwete amwajibishe.

“Mimi siyo Mzaramo. Hiki ni Kiswahili. Sisi wengine kule Usukumani kusema vijimambo, au vijisenti, vijitoto hivi ni kawaida kwa desturi zetu…ndiyo maana napenda kusema wazi kwamba iwapo kuna Watanzania niliwaumiza kwa kauli ile niliyoitoa kwa nia njema kabisa na wala si kwa lengo la kuwakejeli, naomba radhi kwa hilo,” alisema Chenge wakati huo.

Tuhuma dhidi ya Chenge ziliandikwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la The Guardian la nchini Uingereza likikariri taarifa kutoka Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai ya nchini humo (SFO).

Gazeti hilo liliandika kuwa, uchunguzi wa SFO uligundua akaunti moja inayohusishwa na Chenge ikiwa na zaidi ya dola za Marekani milioni moja iliyopo kwenye kisiwa cha Jersey.

Gazeti hilo liliandika kwamba, SFO ilikuwa ikitarajia kuanza upya kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ili kuangalia iwapo zilikuwa na uhusiano na zile zinazoaminika kuwa zilitolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 70, mwaka 2002.

The Guardian katika habari yake hiyo liliripoti kuwa, taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.

Gazeti hilo lilimkariri Waziri Chenge akikiri kwamba fedha hizo ni zake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Jambo la wazi linalotaka kuonekana hapa ni kwamba mimi nilipokea kwa lengo la kujinufaisha mwenyewe fedha za rushwa kutoka BAE. Huu ni uongo,” alisema Chenge.

Aidha, gazeti hilo lilimkariri Chenge akisema kuwa, wakati rada hiyo ilipokuwa ikinunuliwa yeye alihusika kwa kiwango kidogo sana katika mchakato mzima, kwani jambo hilo lilishughulikiwa na wizara nyingine na uamuzi ukaidhinishwa na Baraza la Mawaziri.

Mbali ya hilo, gazeti hilo lilimkariri mwanasheria wa Chenge anayeishi Cleveland, Ohio, nchini Marekani, J Lewis Madorsky, akikanusha kwa niaba ya mteja wake huyo, kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha zake na tuhuma zozote.

“Wakati tukitambua kuwa masuala hayo yalitokea muda mrefu uliopita, tunaweza tu tukathibitisha kuwa, tuhuma zozote za ukiukwaji wa sheria, ukiukwaji wa maadili, kutenda isivyo sawa na mambo mengine ya hivyo dhidi ya mteja wetu ni mambo ambayo kimsingi tunayakanusha kwa nguvu kubwa,” alisema mwanasheria huyo wa Chenge.

Hata hivyo, gazeti hilo liliandika uchunguzi huo dhidi ya Chenge unamfanya yeye kuwa tu shahidi muhimu, kwani wanaielenga zaidi BAE ambayo inadaiwa ilimlipa wakala mmoja wa Tanzania mamilioni ya fedha ili kujenga ushawishi wa rada iliyokuwa ikiiuza kununuliwa.

Wakala huyo ambaye amekuwa akitajwa kwa muda mrefu, na ambaye sasa anaaminika kukimbia nchini na kutafutwa na polisi wa kimataifa ni, Shailesh Vithlani.


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents