Siasa

Chenge sasa abanwa

Waziri ChengeMBUNGE wa Maswa, Bw. John Shibuda (CCM), amemtaka Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, kuelezea tuhuma zinazomkabili, kwamba anamiliki kiasi cha dola milioni moja nje ya nchi..


 



Waziri Andrew Chenge


 


Na Joseph Lugendo, Dodoma




MBUNGE wa Maswa, Bw. John Shibuda (CCM), amemtaka Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, kuelezea tuhuma zinazomkabili, kwamba anamiliki kiasi cha dola milioni moja nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge mjini hapa jana, kuhusu kuwapo kwa tuhuma hizo, Mbunge huyo alisema kimsingi yeye hapingi kuwapo kwa Waafrika matajiri, kwa kuwa hicho ni kielelezo cha uhuru wa kweli walioupigania kutoka kwa Wakoloni.

Hata hivyo, alitahadharisha kwamba dhana ya Watanzania kuwa na mali isigeuzwe mlango wa kuwahujumu wengine na kwamba kufanya hivyo kutakuwa sawa na kutengeneza kundi la wanyonyaji, ambalo lilikataliwa wakati wa ukoloni.

“Tuliwafukuza wanyonyaji si kwa rangi bali kwa tabia, hulka na silka yao na hivyo tuwe makini tusije tukawatengeneza wanyonyaji weusi,” alisema.

Alimshauri Bw. Chenge aeleze jinsi alivyopata fedha hizo, ili kuondoa alichokiita fitina za uzushi na kudhibiti hukumu za hisia.

Naye Mbunge wa Karatu, Dkt. Wilbroad Slaa (CHADEMA), alisema Bw. Chenge alikuwa mtumishi wa Serikali na kwamba anafahamu mshahara, posho na safari alizopata na kusisitiza umuhimu wa Waziri huyo kujieleza.

Aliitaka Serikali kwa upande wake, ifanye uchunguzi makini dhidi ya tuhuma hizo, kwa kuwa fedha hizo ni nyingi na kuongeza kuwa zingeweza kujenga zahanati au shule za sekondari kila kata nchi nzima, bila kuchangisha wananchi.

Alibainisha kuwa anafuatilia taarifa nyingine kuhusu umiliki wa fedha za viongozi wengine nje ya nchi na kuitaka Serikali ifunge akaunti za nje za viongozi hao.

Kuhusu kurejea kwa wabunge wa CUF bungeni jana, Bw. Slaa alisema haoni hoja hapo, kwa kuwa kama ni adhabu itolewe kwanza ndipo watakapojadili hoja.

Alisema anashangaa Spika wa Bunge, Bw. Samwel Sitta, kutangaza kutoa adhabu ya kuwanyima posho wakati ni jambo la kawaida, kwa kuwa Mbunge asipokuwa bungeni hapati posho.

Aidha alisema tangazo la adhabu hiyo ya Spika limemfanya aanze kuhoji iwapo Bw. Sitta alikuwa akitoa posho kwa baadhi ya wabunge wawapo nje ya Bunge.

Naye Reuben Kagaruki, anaripoti kwamba Chama cha Wananchi (CUF) kimeitaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kuchukua hatua za kisheria haraka na kumfungulia kesi Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, kutokana na taarifa kuwa akaunti yake nje ya nchi imekutwa na sh. bilioni moja.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema huu ni wakati muafaka kwa Rais Jakaya Kikwete, kumchukulia hatua Bw. Chenge, kwani kwa muda wake wa utumishi hakustahili kuwa amejipatia kiasi hicho.

“TAKUKURU inawajibika kumfungulia mashitaka ya ufisadi kwa kuzingatia kifungu cha 29 cha sheria ya kuzuia rushwa ikiwa maelezo aliyotaja kueleza mali alizonazo hakutaja akaunti yake ya Jersey,” alidai Profesa Lipumba.

Alisema anavyofahamu Bw. Chenge alihitimu katika Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1972 na kuajiriwa na Serikali kama mwanasheria. Baada ya hapo alikwenda kusoma Shahada ya pili katika chuo cha Havard, Marekani na mwaka 1975 alirejea na kuendelea na kazi serikalini.

Alipandishwa hadi akateuliwa kuwa Mwanasheria wa Serikali mwanzoni mwa miaka ya 1990 hadi 2005. Alisema baada ya uchaguzi mkuu, aliteuliwa kuwa Waziri wa Afrika Mashariki katika Serikali ya Rais Kikwete na baadaye kuhamishiwa Wizara ya Miundombinu.

Profesa Lipumba alisema kwa mshahara na marupurupu ya Serikali haiwezekani akalimbikiza dola milioni moja katika akaunti yake, hivyo akatoa mwito kwa TAKUKURU iwajibike kumchukulia hatua mara moja.

Alisema kulingana na gazeti la Guardian la Uingereza kuwa Mwanasheria wake J Lewis Madorky wa Cleveland, Ohio, Marekani, gharama za wakili wa Marekani ni kubwa mno hivyo mfanyakazi wa Tanzania anayeishi kwa mshahara na marupurupu ya Serikali, hawezi kumudu gharama za wakili kutoka huko.

Alisema wakili wa Marekani hutoza dola 200 kwa saa. “Tuhuma zilizopo bila shaka Rais Kikwete alikuwa na taarifa hizo na zilitosha kutomrejesha Bw. Chenge katika Baraza la Mawaziri pale alipofanya mabadiliko,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema kwa kuwa Bw. Chenge hajakanusha, Rais Kikwete inabidi amwachishe uwaziri na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Profesa Lipumba alisema sheria ya maadili ya viongozi inawataka wabunge kutoa taarifa ya mali walizonazo kila mwaka na zinapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kina na TAKUKURU.


 


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents