Habari

Chifu Fundikira afariki dunia

MWANASIASA mkongwe na Chifu wa kabila la Wanyamwezi, Abdallah Said Fundikira, amefariki dunia.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima


MWANASIASA mkongwe na Chifu wa kabila la Wanyamwezi, Abdallah Said Fundikira, amefariki dunia.


Habari zilizopatikana mjini hapa, zilieleza kuwa, Chifu Fundikira alifariki dunia tarehe 6 mwezi huu majira ya saa 7:30 mchana nyumbani kwake Mwanza Road, kutokana na shinikizo la damu na umri mkubwa. Hadi anafariki alikuwa na umri wa miaka 86.


Habari kutoka kwa wanafamilia zinaeleza kuwa, marehemu Chifu Fundikira aliyekuwa waziri mweusi wa kwanza wa sheria, atazikwa leo Jumatano, katika makaburi ya machifu ya Itetemya, yaliyopo katika eneo la Kipalapala.


Taarfa hizo zilieleza kuwa, mazishi hayo yatafanyika kati ya saa 12:30 jioni na saa 1:00 jioni kama taratibu za mazishi ya machifu wa Kinyamwezi zinavyoelekeza.


Chifu Fundikira atakumbukwa kama mmoja wa watu ambao wameshiriki siasa kabla Tanganyika haijapata uhuru akiwa miongoni mwa weusi wa mwanzo kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria.


Fundikira pia alikuwa miongoni mwa weusi wa kwanza wasomi kusomea masuala ya sheria yaliyompa fursa kuwa miongoni mwa mawaziri katika baraza la kwanza chini ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kabla ya kupoteza madaraka yake miaka michache baadaye baada ya kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili ya uongozi.


Aidha, mwanasiasa huyo ambaye aliendelea kuwa nje ya shughuli za kisiasa alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kabisa na mwasisi wa mageuzi miaka ya mwanzo ya 1990, pale aliposhiriki kikamilifu katika kuanzisha Vuguvugu la Mageuzi (NCCR) akishirikiana na kina Mabere Marando, Christopher Mtikila, na wengine wengi.


Hata hivyo muda mfupi baadaye alitofautiana kimwelekeo na wenzake akiwa mwenyekiti wao, baada ya kutangaza dhamira yake ya kufanya vuguvugu hilo la NCCR kuwa chama cha siasa hata kabla ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa rasmi Julai mwaka 1992.


Tofauti hizo zilimfanya Fundikira akishirikiana na wanasiasa wengine kuunda chama chake cha United Democratic Movement (UMD) na kikawa miongoni mwa vyama vya kwanza vya siasa vya upinzani hapa nchini, kikijulikana sana kwa sera zake za majimbo.


Baada ya kukaa upinzani kwa muda, alirejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambako aliteuliwa na mwanzoni mwa miaka ya 2000 akateuliwa na aliyekuwa Rais Benjamin Mkapa kuwa mbunge wa kuteuliwa nafasi aliyokuwa nayo hadi mwaka 2005.


Baada ya kumaliza awamu hiyo ya ubunge, Fundikira aliamua kurejea nyumbani kwake Tabora ambako aliishi hadi anafariki dunia jana.


Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Fundikira aliyezaliwa Februari 2, mwaka 1921, alikuwa ni chifu wa tatu wa Unyanyembe aliyetawazwa mwaka 1957 na akaendelea na wadhifa huo hadi mwaka 1962 wakati Serikali ya Tanzania ilipofuta uchifu.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents