Siasa

Chuo Kikuu Dar chafungwa

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani kimewasimamisha masomo kwa muda usiojulikana wanafunzi wote wanaochukua shahada ya kwanza kutokana na kugoma kuingia madarasani kwa wiki moja

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani kimewasimamisha masomo kwa muda usiojulikana wanafunzi wote wanaochukua shahada ya kwanza kutokana na kugoma kuingia madarasani kwa wiki moja.

Taarifa iliyotolewa jana asubuhi chuoni hapo na Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala ilisema wanafunzi wengine wanaochukua shahada ya uzamili, udaktari (PhD), kozi fupi na wageni kutoka nje ya nchi wataendelea na masomo kama kawaida.

Agizo la kuwasimamisha wasomi hao liliwataka wawe wameondoka mara moja eneo la chuo na hosteli zao za Mabibo zilizopo jijini Dar es Salaam.

Aidha, taarifa hiyo ilifafanua kuwa sababu ya kufunga chuo hicho ni kutokana na wanafunzi hao kugoma kuingia madarasani pamoja na kuendelea kufanya vurugu ambazo zilikuwa zinahatarisha amani katika eneo la chuo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia magari ya polisi ya kumwaga maji ya kuwasha na askari wenye bunduki wakiwa wametanda maeneo mbalimbali ya chuo.

Baada ya kutolewa tangazo hilo na kubandikwa katika mbao za matangazo chuoni hapo, wanafunzi walionekana wakiwa kwenye harakati ya kuondoa mizigo yao ili waondoke.

Kutokana na agizo hilo kuwataka kuondoka mara moja polisi walionekana wakifuatilia kwa karibu wanafunzi hao ili kuhakikisha wanabeba mizigo yao na kuondoka.

Katika hosteli za Mabibo, Nipashe ilishuhudia baadhi ya wanafunzi hao wakiwa na majonzi wakati wakihamisha mizigo yao.

Hata hivyo, wengine walionekana wakiingia hapo wakiwa wamejazana kwenye magari huku wakiimba EPA, EPA, EPA wakiimanisha Akauti ya Madeni ya Nje.

Aidha, walisikika wakisema kuwa kama mafisadi wasingeiba fedha za EPA zingetosha kuwasomesha, lakini hivi sasa wanafukuzwa kama wakimbizi wakati wakidai mkopo wa asilimia 100.

Baadhi ya wanafunzi hao walionekana wakipita katika maeneo ya chuo na hosteli za Mabibo huku wakiongea wenyewe kama watu waliorukwa na akili.

Akizungumza na Nipashe, Naibu Mkuu wa Makamu wa Chuo ambaye anashughulikia utawala, Profesa Yunus Mgaya alisema, chuo hicho kimewatimua wanafunzi hao kwa maagizo ya Baraza la chuo hicho.

Alisema mwanafunzi yoyote atakayekaidi agizo la kuondoka hapo atakumbana na polisi ambao muda wote walikuwa wakirandaranda eneo la chuo na magari yao.

Aidha, Profesa Mgaya alisema, wanafunzi wa Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (IJMC) ambayo ipo chini ya chuo hicho hawakuguswa na adhabu.

Alisema wanafunzi hao wa IJMC waliandika barua mapema kwa uongozi wa chuo kuwataarifu kwamba hawashiriki katika mgomo.

Kwa upande wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha jijini Dar es Salaam, (Duce) alisema, adhabu hiyo pia haitakihusu.

Hata hivyo, alikiri kwamba Duce jana asubuhi kulikuwa na mgomo na kwamba kama wataendelea hatua zaidi kama zilizochukuliwa na chuo kikuu sehemu ya mlimani zitachukuliwa pia kwao.

“Duce kipo chini ya chuo hiki, lakini kinatawaliwa na bodi ya magavana hivyo siwezi kukitolea maelezo zaidi ila taarifa nilizonazo jana walikuwa na mgomo,“ alisema.

Akizungumzia Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa nacho alisema kulikuwa na mgomo, lakini hatua za kuwatimua wanafunzi wake bado hazijachukuliwa.

Akizungumza na Nipashe jana asubuhi Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Antony Machibya, alisema kuwatimua wanafunzi sio suluhisho la madai yao.

Alisema ukweli unabakia pale pale kwamba Serikali ina jukumu la kuwapatia mkopo kwa asilimia 100 bila kujali madaraja wala familia wanazotoka.

Alisikitishwa na kitendo cha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe kuwapa ahadi hewa kwamba atamtuma mtu ili akazungumze nao, lakini juzi jioni wakashangaa kuona akitangaza kwenye televisheni na kuwataka waingie madarasani.

Alisema Daruso ilionana na Profesa Maghembe juzi na kumueleza madai yao ambapo aliahidi kumtuma mtu ili akutane nao, lakini akawadanganya.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ya Profesa Maghembe kuwakacha, Daruso itamtafuta Rais Jakaya Kikwete ili kumpa malalamiko yao baada ya kubaini kuwa wengine wote ni wababaishaji na hawawezi kutatua matatizo yao.

Akizungumza juzi, Profesa Maghembe, alisema sera ya uchangiaji wa elimu ya juu haiwezi kubadilika kwa haraka kama wanavyotaka wanafunzi hao.

Alisema sera hiyo ilipitishwa na Bunge na kwamba ili iweze kubadilishwa lazima ipitie huko.

Akizungumza wakati akiahirisha Bunge wiki iliyopita Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa asilimia 100 ni kitu kisichowezekana.

Utaratibu wa sasa baadhi ya wanafunzi wanapata mkopo kwa asilimia 60, 80 na wengine wasikuwa na uwezo wanapata kwa asilimia 100.

 

Source: Nipashe

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents