Habari

Chupuchupu wafe jirani na Zimamoto

Watu 10, wakiwemo wanafunzi wanne wamenusurika kufa baada ya nyumba yao iliyo karibu na kituo cha Zimamoto Uwanja wa Ndege Zanzibar, kuteketea kwa moto.

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar



Watu 10, wakiwemo wanafunzi wanne wamenusurika kufa baada ya nyumba yao iliyo karibu na kituo cha Zimamoto Uwanja wa Ndege Zanzibar, kuteketea kwa moto.


Moto huo ulianzia katika chumba wanacholala watoto saa 12:30 jioni.


Nyumba hiyo ipo mtaa wa Kiembesamaki, nje kidogo ya mji wa Zanzibarna inamilikiwa na Bi. Fatma Hussein.


Mama mwenye nyumba Bi. Hussein alisema moto huo wakati unawaka, watoto waliokuwemo ndani pamoja na bibi yao, Bi. Mtumwa Hussein (70), ambaye amepooza.


Alisema baada ya moto huo kuonekana, aliwatuma wajumbe wawili kutoa taarifa katika Kituo cha Zimamoto Uwanja wa Ndege kilichopo masafa mafupi ili wapate msaada, lakini walijibiwa hawawezi kutoa huduma hiyo mpaka wapate maelekezo kutoa Makao Makuu.


“Mjumbe wa kwanza alipofika alielezwa kwamba, huduma ya zimamoto haiwezi kupatikana kwa wakati huu mpaka wapate amri kutoka Makao Makuu,“ alisema Bi Fatuma.


Alisema baada ya kupokea kauli hiyo aliamua kuwasiliana na bosi wake, ambaye ni Meneja wa Shirika la Posta Zanzibar, Bi. Fatma Bakar, kuomba msaada zaidi, lakini hakuweza kufanikiwa.


Mama huyo alisema majirani walifanikiwa kumtoa mama yake Bi. Mtumwa, kutoka ndani na kumhamishia nyumba ya jirani pamoja na watoto, lakini vitu vyote viliteketea.


“Inasikitisha sisi wananchi tunalipa kodi, lakini inapotokea janga kama hili tunashindwa kupewa huduma kwa wakati, na hasa hapa kwetu ambapo Zimamoto wako jirani,“ alilalamika mama huyo ambaye ni mfanyakazi wa Shirika la Posta.


Alisema kiongozi wa Serikali ya Mtaa huyo Sheha, pia alifanya juhudi za kuwaita askari hao wa zimamoto, lakini hawakuweza kufanikiwa kutokana na kuendelea kutetea msimamo wao wa kutotoa huduma hadi wapate maelekezo ya makao makuu.


Mama huyo alisema baada ya tukio hilo, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Bw. Mansour Yussuf Himid, alifika katika eneo la tukio, lakini nyumba hiyo ilikuwa ikiendelea kuwaka huku wananchi wakiendelea kuzima kwa kutumia ndoo za maji bila ya mafanikio.


Alisema hadi jana hakuna mafundi wowote kutoka Shirika la Umeme waliofika nyumbani hapo kujua chanzo cha moto huo.


Alisema kabla ya moto huo kutokea umeme ulikuwa ukiwaka na kukatika na anawasi wasi mkubwa kuwa ndio chanzocha nyumba hiyo kuteketea.


Polisi walichukua maelezo, juu ya mazingira ya tukio lakini hadi sasa familia yake ya watu 10 inalazimika kuishi kwa majirani, ikiwemo watoto wanne ambao wanasoma.


Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto Zanzibar, Bw. Ali Abdalla Malimusi, alisema hawezi kuzungumzia lolote kuhusiana na tukio hilo kwa vile yuko likizo.


Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Mgharibi, Bw. Said Marekano, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi inafanya uchunguzi.


Habari kutoka katika eneo la tukio zilisema kwamba wakati nyumba hiyo ikiwa imeungua kwa kiasi kikubwa kulitokea gari mbili za Kikosi cha Valantia zenye namba za usajili KVZ 223 iliyokuwa imebeba tangi la maji na nyengine KVZ 219 iliyokuwa na jenereta.


Hata hivyo wakati magari hayo yakifika katika eneo hilo nyumba hiyo ilikuwa tayari imekwishateketea na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh. milioni 40.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents