Corona: Wanafunzi walioomba kurudi Tanzania wabaki China – Balozi Kairuki

BALOZI wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema maombi ya baadhi ya wanafunzi wanaosoma nchini humo, kutaka kurejeshwa nyumbani, lazima yafanyike kisayansi, kwa utaratibu utakaohakikisha ugonjwa utokanao na virusi vya corona hauletwi nchini.

Aidha, amewaomba wazazi wa wanafunzi hao walioko China, kuepuka kuwatia hofu, badala yake wawatie moyo, kwa kuwa mazingira waliyomo ya kufungiwa kuepuka maambukizi ya corona ni sawa na ya vita.

Balozi Kairuki amesema hayo jana kwenye mahojiano kati yake na Televisheni ya Clouds ya jijini Dar es Salaam, kuhusu baadhi ya wanafunzi kutoka mji wa Wuhan, waliojitokeza kupitia mitandao ya kijamii, kuomba Serikali ya Tanzania iwarejeshe nchini.

“Ni kweli nimeona video ya vijana wetu, wakituma ujumbe wakitaka waondolewe pale Wuhan… vijana walichukua hatua ya kukusanyika, ambayo ni makosa. Nitoe rai, wasifanye walichofanya kwa kuwa wanajihatarisha maisha yao,” amesema Balozi Kairuki.

Alisema rai hiyo ya kutaka kurejeshwa nyumbani, walishaileta rasmi na ubalozi ukaifanyia kazi, kupitia mamlaka zinazohusika upande wa serikali ya China na serikali ya Tanzania.

Hata hivyo, Balozi Kairuki alisema, “Mambo haya hayatakiwi kufanywa kwa mihemko. Lazima yafanyike kisayansi, yafanywe kwa taratibu ambazo zitahakikisha usalama wao na usalama wa wengine watakaohusika na kuchukua hatua hiyo.”

“Tutakapofika mahala, tathimini ikafanyika kwamba tunaweza kufanya hili zoezi kwa uhakika na kitaalamu na kwa usalama, naamini serikali ni sikivu itachukua hatua zile zinazozingatia maslahi ya taifa.”amesema.

Alisema ubalozi umejifunza kutoka kwa mataifa mengine, yaliyojaribu kuwaondoa wanafunzi yakasababisha maambukizi zaidi ya corona. Alitoa mfano wa Japan kwamba ilikuwa na wanafunzi Wuhan, ambao wote hakuna aliyekuwa ameambukizwa virusi hivyo.

Kwa mujibu wa Kairuki, wakati wa kuwaondoa nchini China, wanafunzi watano waliambukizwa virusi vya corona na waliwaambukiza wengine watano, waliosafiri nao kurudi nyumbani.

Walipofika nchini kwao, katika mchakato wa kuwapeleka eneo la karantini katika kiwanja wa ndege, wapo wafanyakazi wa kiwanjani pia waliambukizwa. Matokeo yake idadi ya wagonjwa wa corona walioko Japan, imeongezeka hadi watu wapatao 20.

“Makosa waliyofanya Japan, hatutaki kuyarudia. Hatutaki sisi kufanya uamuzi wa kuchukua hatua bila kujipanga vizuri na matokeo yake tukapeleka ugonjwa nchini kwetu. Lazima tuangalie hili jambo kwa busara na hekima kuhakikisha usalama wa vijana wetu ni nini,” alisema Kairuki.

Akisisitiza umuhimu wa serikali ya Tanzania, kuchukua tahadhari, Balozi Kairuki alisema, “Wenzetu China wana fedha nyingi, wana raslimali nyingi, wana madaktari…unaona wamejenga hospitali kubwa kabisa ndani ya wiki moja, sisi raslimali hizi hatuna.”

“Kama wenye fedha wanapambana hivi na bado mapambano yanaendelea, sasa kwenye nchi zetu za Afrika, lazima tuwe makini kuhakikisha tunachukua kila aina ya hatua kuhakikisha ugonjwa hauji kwenye Bara la Afrika. Tuwalinde watu wengi zaidi,” alisema.

Akitoa rai kwa wazazi wa watoto walioko nchini China, Balozi Kairuki alisema anafahamu wengi wanapitia wakati mgumu, kwa sababu ya watoto wao kuwa katika mazingira, ambayo hawana uhakika nayo na pia kutokana taarifa za mitandaoni zinazotisha.

Alisema kwa sasa usalama wa wanafunzi na raia wote wa Tanzania walioko nchini humo, utatokana na kufuata masharti ambayo watu wote wamepewa wayazingatie.

Alisema raia wa Tanzania walioko China husuani katika mji wa Wuhan, idadi yao ni 437 na hakuna aliyeambukizwa.

Akielezea mazingira wanayopitia Watanzania walioko Wuhan, Kairuki alisema si ya kawaida, kwani wamefungiwa kwa wiki mbili, hawawezi kutoka nje ya mji, nje ya eneo la makazi au nje ya bweni.

Alisema mazingira hayo, yamesababisha watu wakiwamo wanafunzi kuwa na msongo wa mawazo. Alisema ubalozi umeendelea kuwasiliana na wanafunzi kupitia jumuiya zao ;na penye changamoto unakabiliana nazo.

Baada ya picha za wanafunzi wa Tanzania walioko China kuonekana mtandaoni, wakiomba serikali iwarudishe nyumbani, kumekuwapo maoni kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo waliotaka serikali kutoa tamko na wengine wakitaka ifanye utaratibu, kuwarejesha haraka kuwaeupusha na hatari ya ugonjwa.

Katika hatua nyingine, Chama cha Watanzania Waliosoma China (CAAT) kupitia kwa mwenyekiti wake, Dk Liggy Vumilia, kimeeleza masikitiko ya janga hilo lililoikumba nchi hiyo.

Kimeunga mkono hatua zinazochukuliwa na serikali ya China, kuwalinda wananchi dhidi ya ugonjwa huo, ambao Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa janga la kimataifa.

Kwa mujibu wa Balozi Kairuki, hadi jana idadi ya watu walioambukizwa na virusi corona walikuwa 42,708. Waliokuwa wameambukizwa na kutibiwa ni 3,998 na waliopoteza maisha ni 1,071.

Hata hivyo, alisema yapo matumaini makubwa, kwani juhudi zinazofanywa na serikali ya China kudhibiti ugonjwa huo, zimeanza kuzaa matunda.

Alisema maambukizi mapya yanapungua na idadi ya wanaopona, inaongezeka.

Kwa siku tano mfululizo, takwimu zinaonesha nje ya mji wa Wuhan, ambako ndiko ugonjwa huo ulianzia, maambukizi mapya yanaendelea kupungua kwa asilimia 50.

Februari 3 mwaka huu maambukizi yalikuwa 890 na juzi yalifikia 444. Alisema sababu kubwa ni juhudi zinazofanywa na mamlaka nchini humo na wananchi kufuata taratibu na miongozo ya kujikinga inayotolewa na serikali.

Source: Habari LEO

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW