Siasa

CUF wamgeuka Lipumba

KUNA kila dalili sasa kuwa, upepo wa kisiasa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, ndani ya chama hicho, umeanza kuchafuka.

na Irene Mark


KUNA kila dalili sasa kuwa, upepo wa kisiasa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, ndani ya chama hicho, umeanza kuchafuka.


Dalili hizo zinaonyesha kuwa, Prof. Lipumba sasa anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanachama wa chama hicho, na iwapo hali ya mambo itaendelea kama ilivyo sasa, huenda mwisho wa mwanasiasa huyo ndani ya chama hicho ukawa mbaya.


Upinzani anaokabiliana nao Prof. Lipumba, unatokana na maamuzi ya pamoja na viongozi wa CUF kupingana na matakwa ya baadhi ya wanachama, ya jinsi mazungumzo ya kutafuta muafaka wa kisiasi visiwani Zanzibar yanavyoendeshwa.


CUF, kwa muda mrefu sasa iko katika mazungumzo na chama tawala, CCM, juu ya muafaka wa hali ya kisiasa kisiwani Zanzibar.


Wakati msimamo wa viongozi hao chini ya Profesa Lipumba, umekuwa kuendelea na mazungumzo ya kutafuta muafaka, baadhi ya wanachama wa chama hicho wanaipinga hatua hiyo, na wanawataka viongozi wao wajitoe katika mazungumzo hayo.


Tofauti hizo baina ya viongozi na wanachama, jana zilionekana kuchukua sura mpya, yenye dalili za wazi za wanachama kuwachoka viongozi baada ya kukataa kumsikiliza Profesa Lipumba na kumfungia ndani ya ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari.


Profesa Lipumba aliyetimiza umri wa miaka 55, Juni 6, mwaka huu, alijikuta katika dhahama hiyo wakati akitoka nje ya ofisi za makao ya CUF na kukutana na umati mkubwa wa wanaCUF walioanza kumtuhumu kuwa yeye pamoja na viongozi wenzake wa chama hicho wanahujumu wanachama katika mazungumzo ya kutafuta muafaka.


Akiwa mwenye furaha baada ya kutoa tamko la Baraza la Uongozi la CUF kuhusu mazungumzo ya muafaka yanayoendelea kati ya chama hicho na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Lipumba, mzaliwa wa Kijiji cha Ilolangulu, Tabora, alijikuta katika madhila ya kuzomewa na kufungiwa geti na wanachama wapatao 300 waliokuwa wamekusanyika nje ya ofisi hizo.


WanaCUF kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini, pia waliwazuia viongozi wengine waliokuwa wameongozana na Profesa Lipumba kutoka ndani ya ofisi hizo hadi watakapowathibitishia kuwa wamekubali kutekeleza matakwa yao ya kukitoa chama chao katika mazungumzo ya kutafuta muafaka.


Wakionekana wenye jazba na hasira, wanachama hao walidai kuwa, mazungumzo hayo hayana mwelekeo wenye nia ya kumaliza mgogoro wa kisasia visiwani Zanzibar.


Walikuwa wakipaza sauti zao, wakiwataka viongozi wao, akiwemo Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kutoendelea na mazungumzo ya muafaka na kwamba wapo tayari kujibu lawama, itakapowalazimu kufanya hivyo.


Katika hali ambayo hakuitegemewa, na ambayo ilionekana dhahiri kumshangaza Profesa Lipumba pamoja na wenzake, walijikuta wakikabiliana na mmoja wa wazee wa CUF, aliyejitambulisha kwa jina la Mussa, ambaye alianza kuwatuhumu kwa sauti ya juu kuwa mwenyekiti na katibu wa chama hicho wanawahujumu wanachama kwa kufanya mazungumzo yasiyo na mwisho, mwelekeo wala faida kwao.


“Tunajua kuwa ninyi viongozi wetu mnatuhujumu, huu ni muafaka wa tatu, lakini hakuna dalili za kueleweka, tunaona tu mnakaa vikao visivyo na mwisho nyie…, huku sisi tunataabika.


“Maalim jitoe kwenye mazungumzo hayo, …sisi ni waajiri wenu, na ndio wenye chama, kwa kuwa sera yetu inasema chama ni mali ya wanachama, hivyo basi tupo tayari kujibu lolote kwa ajili yenu, lakini mkishakatisha mazungumzo hayo.


“Waswahili husema kikulacho ki nguoni mwako, wewe mwenyekiti na katibu mnavuruga chama, tunakosa imani juu yenu,” alituhumu mzee Mussa mbele ya Lipumba na viongozi wengine wa chama hicho, akiwemo Maalim Seif.


Prof. Lipumba akiwa ameandamana na baadhi ya viongozi wenzake, alijaribu kuwasihi wanachama hao kupunguza jazba ili wamsikilize, jambo lililopingwa na wanachama hao ambao walianza kumzomea huku wakipiga kelele za kumtaka asitishe mazungumzo ya muafaka.


“Hakii…,” alisema Prof Lipumba kabla ya kuanza kuwasihi wanachama wake, lakini hata hivyo alijibiwa tofauti na ilivyozoeleka.


“Hakuna haki hapa, tunataka mjitoe kwenye muafaka, vinginevyo tutajua cha kufanya, hapa haki hakuna,” walipiga kelele wanachama hao.


Prof. Lipumba akiwa ameandamana na Maalim Seif, walilazimika kurudi ndani ya ofisi na kufanya kikao cha dharura wakiwa wamejifungia bila kuruhusu mtu yeyote kusogelea chumba hicho, wakiwemo waandishi wa habari.


Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Prof Lipumba alisema Baraza la CUF limemtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa kauli yake kuhusu maneno ya uchochezi yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, alipotembelea kisiwani Pemba kwa ajili ya mazungumzo ya muafaka na kuangalia hali ya kisiasa nchini.


Alisema baraza hilo limesema, maneno ya Makamba yameongeza mpasuko wa kisiasa na kuvuruga dhamira njema ya kufanikisha muafaka wa kudumu wa kisiasa visiwani humo, hali inayohatarisha amani na utulivu.


Profesa Lipumba amekuwa mwenyekiti na mgombea wa urais kupitia chama hicho tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.


Katika uchaguzi wa mwaka 1995, alishika nafasi ya tatu, akivuna asilimia 6.43 ya kura zote, huku Benjamin Mkapa akiingia Ikulu kwa tiketi ya CCM akimrithi Ali Hassan Mwinyi ‘Mzee Ruksa’.


Na hata alipoingiza kwa mara ya pili kete yake ya urais mwaka 2000, Profesa Lipumba alikwama kwa Mkapa, ambako alishika nafasi ya pili kwa kuvuna asilimia 16.26 ya kura zote kabla ya mwaka 2005 kuvuna asilimia 11.68, hivyo kumweka katika nafasi ya pili kinara akiwa rais wa sasa, Jakaya Mrisho Kikwete aliyeingia madarakani kwa ‘gia’ ya ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’, ingawa mpaka sasa akiingia katikati ya awamu yake ya kwanza ya miaka mitano, hakuna kinachoelekea kufanana na ‘gia’ hiyo.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents