Habari

CUF ya Lipumba yamlipua Mbunge Mtolea aliyejiuzulu, wadai ulikuwa ni mpango

Chama Cha Wananchi (CUF) kimesema sababu alizozitoa aliyekuwa mbunge wake wa Temeke, Abdallah Mtolea aliyetimkia CCM, hazina sababu na alilenga kuhalalisha kitendo chake cha kuwa mmoja wa watu wanaosajiliwa na chama tawala.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Novemba 16, 2018 na Abdul Kambaya ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CUF upande wa mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Jana mchana Alhamisi Bungeni jijini Dodoma, Mtolea alitangaza kujivua nyadhifa zake ndani ya chama hicho cha upinzani na jioni akaomba kujiunga na CCM na kupokelewa.

Mtolea alitaja sababu tatu zilizomsukuma kuchukua uamuzi huo kuwa ni kukosa ushirikiano ndani ya chama, migogoro ndani ya chama na kwamba alipata taarifa kwamba atafukuzwa uanachama.

Hata hivyo, Kambaya amesema hoja hizo hazina mashiko na alijaribu kutaka kuhalalisha kitendo chake cha kuwa mmoja wa watu wanaosajiliwa na CCM

Kuhusu kukosa ushirikiano ndani ya chama, Kambaya amesema si kweli kwa sababu mbunge akichaguliwa anapaswa kushirikiana zaidi na wananchi katika jimbo lake analoliongoza.

“Hii ni hoja dhaifu sana, lini alitaka ushirikiano wa chama akaukosa? Baada ya mbunge kuchaguliwa anatakiwa kujenga ushirikiano na wananchi katika jimbo lake, sasa yeye anataka ushirikiano upi ndani ya chama?” Amehoji Kambaya.

Akizungumzia mgogoro ndani ya chama hicho, Kambaya amesema migogoro haiwezi kumwondoa mtu ndani ya chama kwa sababu kila chama kina migogoro yake lakini bado vyama vipo na vinaendelea kuwepo.

Kuhusu mikakati ya kumfukuza uanachama, Kambaya amesema Mtolea ni mmoja wa watu waliokuwa wanasema hawautambui upande wa Profesa Lipumba, hivyo anashangaa kuwa na wasiwasi na upande ambao haumtambui mpaka akajivua uanachama.

“Mtolea ameshindwa kuonyesha hata barua ya wito wa kamati ya maadili, hana barua hiyo. Tatizo tulilonalo sasa ni wabunge kutaka vyeo, wanadhani nao watapewa uwaziri kama (Mwita) Waitara (Naibu Waziri Tamisemi),” amesema Kambaya.

Kuhusu suala la korosho, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Jafar Mneke amesema chama hicho kinaunga mkono hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kununua korosho za wakulima kwa Sh3,300 kwa kilo kwa sababu hatua hiyo inalenga kumuinua mkulima.

Ameishauri Serikali kuweka mipango mizuri ya kuwanufaisha wakulima katika misimu ijayo ya kilimo.

Amesema anaamini wakulima watalipwa fedha taslimu tofauti na ilivyokuwa kwenye mpango wa stakabadhi ghalani.

“Serikali haitakuwa inanunua korosho kila msimu, hii imefanyika kwa dharura tu. Kwa hiyo, Serikali na bodi za mazao mbalimbali zitafute masoko ya mazao ya wakulima sambamba na kujenga viwanda vinavyotumia malighafi za mazao,” amesema Mneke.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents