Habari

Cyril Ramaphosa aapishwa rasmi kuwa rais wa Afrika ya kusini, viongozi wengi wahudhuria akiwemo rais Magufuli wa Tanzania (+ Video)

Cyril Ramaphosa aapishwa rasmi kuwa rais wa Afrika ya kusini, Rais Magufuli ahudhuria (+ Video)

CYRIL RAMAPHOSA ameapishwa leo kuwa Rais wa Afrika Kusini kwa kipindi cha miaka mitano ijayo akiwa anakabiliwa na jukumu la kupiga vita rushwa katika serikali.

Ameapishwa katika uwanja uliokuwa na watu wapatao 30,000  katika mji mkuu wa nchi hiyo, Pretoria, wakiwemo viongozi kadhaa kutoka nchi jirani za Congo, Zimbabwe, Mozambique, Tanzania na kadhalika.

 

Kuapishwa kwake kunafuatia ushindi wa chama chake cha African National Congress kilichopata ushindi wa asilimia  57.5 katika uchaguzi wa mwezi uliopita. Katika uchaguzi huo, chama hicho kilipata ushindi mdogo zaidi tangu chaguzi zilizofuatia baada ya kukomeshwa kwa ubaguzi wa rangi nchini humo mwaka 1994.

Ramaphosa alichukua nafasi hiyo baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma, alishinikizwa kujiuzulu kutokana na kashfa za rushwa, jambo ambalo lilikidhoofisha vibaya chama cha ANC.

Akiwa mfuasi thabiti wa rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo,  Nelson Mandela, Ramaphosa anatarajiwa kuishafisha serikali ya nchi hiyo na kufufua umaarufu wa chama tawala.

“Bila yeye, ANC ingepata asilimia 40 tu ya kura zote,” alisema hivi karibuni mmoja wa viongozi wa chama hicho, Fikile Mbalula.

Zuma hakuwepo katika hafla hiyo kutokana na madai yake kwamba hakufanya kosa lolote lililomfanya kung’olewa nafasi yake.

Wakati wa uchaguzi Ramaphosa aliahidi kuendeleza vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, vitu ambavyo huvuruga uchumi wa nchi hiyo ambayo imeendelea zaidi kuliko nchi zote zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.

 

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents