Dar kuzizima tena

Dar kuzizima tena
Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) leo kuanzia saa tisa
alasiri litalipua masalia ya mabomu yaliyobaki katika mlipuko uliotokea
Aprili 29 mwaka huu, ili kuepusha uwezekano wa mabaki hayo kuleta
madhara zaidi

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi
aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ulipuaji huo utafanyika katika
kambi ya JWTZ iliyopo Mbagala, eneo ambalo mabomu ya awali yalilipuka.
Kutokana na uamuzi huo, Mwinyi amewataka wananchi kuanzia muda huo
wakae mita 500 kutoka eneo la kambi hiyo.

Mwinyi alisema shughuli hiyo itafanyika kwa umakini mkubwa ambapo
wataalamu wataanza kwa kutanguliza milipuko miwili midogo kwa ajili ya
kutoa tahadhari kabla ya kuendelea kulipua mabomu hayo mfululizo kwa
muda wa saa mbili. “Baada ya milipuko hiyo miwili, itafuatia milipuko
mingine ya mfululizo ya nguvu kiasi hadi saa 11 jioni, wananchi
wanaombwa wawe umbali wa mita 500 kutoka kambi ya Mbagala,” alisema
Mwinyi.

Mwinyi alisema silaha zitakazoharibiwa ni pamoja na masalia ya
risasi, baruti, viwashio na mabomu ambayo hayakuweza kulipuka siku
ilipotokea ajali. Alisema jumla ya mabomu 75 ya kutupa kwa mkono aina
ya ‘Stick hand grenades’ na dazeni kadhaa za viwashio pamoja na fyuzi
zake vitateketezwa.

Alisema mabomu hayo inabidi yaharibiwe eneo hilo kwa sababu
yanaweza kulipuka wakati wa kuyahamisha na kuleta madhara kwa watu
watakaoyahamisha. Hata hivyo alisema kazi hiyo itafanywa na wataalamu
wa Jeshi na hakutakuwa na madhara yoyote kwa watu kwani yatalipuliwa
kiufundi. “Wizara ya Ulinzi na JKT inapenda kuwahakikishia wananchi
kwamba kazi hiyo itafanyika kwa uangalifu mkubwa na kwa usalama,”
alisisitiza Waziri Mwinyi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Lukuvi aliwataka wananchi
waendelee na kazi zao kama kawaida kwani shughuli hiyo haitaingilia
kazi zao. Lukuvi aliwataka hata wanafunzi waende shule na kusitokee
kisingizio chochote cha wanafunzi au watu kushindwa kwenda kwenye
shughuli zao au shuleni. Naye Mkuu wa Usalama wa JWTZ, Brigedia
Generali Paul Mella, alisema kambi ya Mbagala ina wanajeshi 200 ambao
watasaidia kuwaelekeza wananchi kabla ya kuanza kwa ulipuaji wa mabomu
hayo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents