Burudani

Davido ana asilimia nyingi kwenye mafanikio ya Diamond, kupatana kwao ni habari njema

Mimi nilikuwa mmoja wa watu walioalikwa kwenye uzinduzi video ya kwanza kubwa ya Diamond Platnumz, Number One uliofanyika Serena Hotel jijini Dar es Salaam, mwishoni kabisa mwa August, 2013.

11280156_410610992455593_717158413_n
Davido na Diamond wakiwa pamoja mastaa wengine jijini Durban ambako kunafanyika tuzo za MTV MAMA

Hiyo ndio ilikuwa video ya kwanza ya Diamond kuifanya nchini Afrika Kusini ambapo aliwachukua Ogopa Videos kwa kazi hiyo. Kipindi hicho Diamond alikuwa ana uhusiano na Penny Mwingilwa. Miongoni mwa vitu alivyovifanya siku hiyo ni pamoja na kumfanyia surprise ya nguvu marehemu Mzee Muhidin Maalim Gurumo kwa kumzawadia gari.

Ulikuwa ni uzinduzi wa aina yake, uliofana na kwa kila mtu aliyekuwepo ilikuwa rahisi kuona ishara ya mafanikio makubwa yaliyokuwa mbele ya mtoto huyu wa Tandale.

Mambo yalikuja kubadilika zaidi October 2013 baada ya Davido kuja Tanzania kwenye Fiesta ya Dar es Salaam. Mazungumzo yalifanyika na Davido kukubalika kuibariki remix ya Number One.

Wawili hao walifanya video ya remix hiyo nchini Nigeria chini ya muongozaji Clarence Peters. Baada ya video kutoka, mambo hayakuwa kama zamani tena. Kipindi hicho Davido alikuwa msanii hot sana Afrika na hivyo kwa Diamond kumpata kwenye remix yake kilikuwa ni kitu sahihi alichowahi kukifanya katika maisha yake.

Kabla ya hapo jina la Diamond lilikuwa ni kubwa tayari Afrika Mashariki, lakini si Magharibi. Remix hiyo ikapendwa, audio na video vikaanza kupata airtime kwenye redio za Nigeria, Ghana na Afrika Kusini. Davido akasaidia kumweka kwenye ramani Naseeb Abdul.

Haichukua muda, nominations zikaanza kumiminika. BET Awards, MTV MAMA hadi CHOAMVA. June 2014, Diamond akapata bahati kutumbuiza kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa la tuzo hizo jijini Durban, SA akiwa na Davido.

Kadri muda ulivyokuwa ukienda, Diamond akaanza kuwa mpinzani wa Davido kwenye tuzo nyingi na ‘tension’ ikaanza kuzaliwa. November 29, Diamond akaibuka mshindi wa tuzo tatu kwenye CHOAMVA na kuwa mbele ya Davido ambaye wengi walihisi hakufurahia.

December 2014, kwenye fainali ya Big Brother Africa, ‘bifu’ ikazaliwa. Ushindi wa Idris Sultan ukamfanya Davido atweet ujumbe uliowakasirisha watanzania wengi. ‘And they cheat again.’

Usiku huo huo Diamond akashinda tuzo zingine zilizokuwa zikitolewa jijini Lagos na akajibu dongo la Davido. Kauli ya Davido ikamweka kwenye kitimoto na kuambulia matusi mengi hadi kutukaniwa mama yake. Bifu ikawa kubwa. Duru za chini ya kapeti zikadai kuwa kambi ya Davido ikatangaza vita kwa Diamond. ‘Speculations’ za bifu yao ziliendelea kwa muda mrefu licha ya mameneja wa Diamond, Babu Tale na Salaam kukanusha mara kadhaa kuwa hakuna bifu kati yao.

Nominations za MTV MAMA 2015 zikawarudisha tena wawili hao kwenye ‘tension.’ Katika muda ambao uadui wa Team Diamond vs Team Kiba ulikuwa umepamba moto, Diamond na Davido wakajikuta wakilazimishwa kutoolewana na hadi July 15, 2015 bado wengi tuliamini kuwa Diamond na Davido haziivi.

Picha zilizowekwa jana kwenye Instagram zinazowaonesha Diamond na Davido wakicheka kama vile hakuna kilichowahi kutokea, zimepokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wao.

11356390_915631631812314_1801786851_n

Na kwa wengi wanaoelewa mchango wa Davido kwa Diamond, hiyo ni habari njema kabisa kuwahi kuisikia mwaka huu kuwa wawili hao hawana tena tofauti. Lakini pia imekuwa ni aibu kiaina kwa watu waliokuwa wakijaribu kuwachonganisha zaidi.

Miaka miwili baadaye baada ya kumshirikisha Davido, Diamond amekuwa staa wa mkubwa barani Afrika ambaye kila msanii anatamani kumshirikisha. Ameshafanya collabo na wasanii wakubwa wa nchini humo wakiwemo P-Square, 2 Face, Iyanya, Tiwa Savage, Waje, Bracket, KCEE na wengine. Lakini hakuna anayeweza kupinga kuwa bila Davido, safari ya Diamond kufika hapo alipo huenda ingechukua muda kiasi.

Wawili hawa watatumbuiza tena pamoja Jumamosi hii kwenye tuzo za MTV MAMA na pengine wanaweza kufanya ngoma nyingine – tena awamu hi inaweza kuwa Davido f/ Diamond. Sipati picha ukubwa wa collabo yao ya pili. Ni noma!

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents