Dawa ya ukimwi yagunduliwa

Wanasayansi nchini Marekani wamegundua chembechembe za kinga ambazo zinauwezo mkubwa wa kupambana na kuua virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ambao hadi sasa hauna chanjo wala tiba ya uhakika, ugunduzi huo tayari umethibitishwa na wataalamu mbalimbali, ikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani.

Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vimeripoti kuhusu ugunduzi huo ambao unaelekea kutoa mapambazuko mapya kwa ugonjwa huo hatari ambao umekuwa ukiathiri nguvu kazi sehemu mbalimbali duniani, hususan nchi zinazoendelea.

Wanasayansi hao wa Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID) walieleza katika taarifa yao ya wiki iliyopita kuwa kwenye utafiti huo wamebaini aina mbili za chembechembe zinazoweza kumsaidia binadamu kupambana na virusi vya ukimwi.

Mkurugenzi wa NIAID, Dk Anthony Fauci alizitaja chembechembe hizo za kinga kuwa ni VRCO1 na VRCO2 ambazo utafiti wake umeonyesha kuwa zinaweza kuua virusi vya ukimwi kwa asilimia 90.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) dawa huthibitishwa pale uwezo wake wa kupambana na ugonjwa unapozidi asilimia 60.

Dk Fauci alisema hayo ni mafanikio makubwa ya kisayansi tangu wataalamu mbalimbali duniani waanze kufanya utafiti  wa namna ya kutibu ugonjwa huo.

Alisema chembechembe hizo za kinga hizo  VRCO1 na VRCO2 zinaweza kutumika katika kubaini aina mpya ya chanjo ambayo itamuwezesha binadamu kuwa na kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi.

Kwa namna chembechembe hizo zinavyofanya kazi, alisema, zikitumika kama chanjo, mwili wa anayechanjwa unajenga kinga ambayo inavishambulia virusi vya Ukimwi na kuviua.

“Kwa sasa soko lina dawa za kupunguza nguvu na kasi ya virusi vya Ukimwi kuathiri chembechembe nyeupe za kujikinga na maradhi na hakuna tiba,” alisema Dk Fauci.

“Lakini utafiti huu ni njia mpya ya kuelekea kupata ufumbuzi wa kudumu katika utaalamu wa tiba.”

Hata hivyo, alisema utafiti huo unaweka matumaini zaidi katika kutoa chanjo ingawa baadaye utawezesha kusaidia kupatikana kwa tiba kamili.Jinsi walivyoendesha utafiti huo, Dk Faci alisema walichukua sampuli mbalimbali za damu zenye virusi vya ukimwi kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Katika sampuli hizo, alisema waliweza kupata aina karibu 200 za virusi vya ukimwi na walipozipambanisha na chembechembe za kinga za VRCO1 na VRCO2, virusi vilikufa bila kuathiri chembechembe nyingine za damu.

Hali hiyo aliilezea kuwa inathibitisha kuwa VRCO1 na VRCO2 zina uwezo wa kupambana na aina zote za virusi vya ukimwi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents