Afya

Dawa za nywele zinaweza kusababisha uvimbe Kwenye kizazi

Matumizi ya dawa za kulainisha nywele ama relaxer kwa jina lingine yanazidi kushamiri miongoni mwa wanawake wengi hapa barani Afrika. Hii ni kutokana na imani kuwa ukitumia dawa hiyo iliyo na kemikali hatari zinasaidia kurefusha nywele na kukufanya upendeze zaidi.

Hata hivyo wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinaweza kusababisha uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo nikali huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.

Utafiti umebaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao fibroids au leimyoma. Hizi ni kemikali ambazo hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata harufu yake husababisha kuzalishwa kwa wingi vichocheo aina ya estrogen ambavyo huchangia kuota uvimbe wa fiboida.

Dk Lauren Chipata kutokea manispaa ya ilala amesema kuwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi ambacho mwanamke yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.Utafiti ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.

Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).

Licha ya serikali kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kukataza dawa ambazo sio salama kwa matumizi ya binadamu kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform, bado baadhi ya bidhaa hizo huuzwa na kutumika na binadamu.

Mwaka 2012, Dk Lauren Wise na wenzake nchini Marekani kupitia kwenye jarida la afya la nchini Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au myoma.

Dk Wise anasema aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangalia umri walioanza kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi gani.

Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa upasuaji.

Na Laila Sued

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents