Tupo Nawe

Deni la taifa lafikia Tsh. Trilioni 52, Serikali yaeleza sababu za kuongezeka kwa deni hilo

Serikali imesema hadi kufikia Agosti mwaka huu, Deni la Taifa lilifikia Tsh. Trilioni 52.303 kulinganishwa na Tsh. trilioni 49.283 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango, Alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa na mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya serikali ya mwaka 2020/21.

Deni la serikali hadi Agosti 2019, lilifikia Tsh. bilioni 52,303.04 ikilinganishwa na Tsh. bilioni 49,283.44 Agosti 2018,” amesema Dkt. Mpango.

Kiwango hicho cha ongezeko ni sawa Tsh. Trilioni 3 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Waziri huyo alibainisha kuwa kati ya deni hilo, Deni la ndani lilikuwa Tsh. trilioni 14.075 na Deni la Nje Tsh. trilioni 38.227, akieleza kuwa ongezeko la deni lilichangiwa na kupokewa kwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mpango amesema tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba mwaka jana, ilionyesha Deni la Serikali bado ni himilivu katika muda mfupi, wa kati na mrefu kwa viwango vya kimataifa.

Kuhusu mwenendo wa viashiria vya uchumi, Dkt. Mpango alisema uchumi wa taifa umeendelea kuwa imara, akibainisha kuwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita (2009 – 2018), Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.4 kwa mwaka.

 

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW