Deni la taifa lapaa

DENI la jumla la taifa liliongezeka mwezi Oktoba na kufikia dola za Marekani milioni 6,894 kutoka kiasi cha dola za Marekani milioni 6,453.5 mwezi uliotangulia, ripoti ya hivi karibuni ya Benki Kuu (BoT) inaonyesha.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima


DENI la jumla la taifa liliongezeka mwezi Oktoba na kufikia dola za Marekani milioni 6,894 kutoka kiasi cha dola za Marekani milioni 6,453.5 mwezi uliotangulia, ripoti ya hivi karibuni ya Benki Kuu (BoT) inaonyesha.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya hali ya uchumi iliyowekwa kwenye tovuti ya BoT juzi, hilo ni ongezeko la dola za Marekani milioni 440.5, sawa na asilimia 6.8.


“Ongezeko hilo linatokana na madeni mapya, kubadilika kwa viwango vya ubadilishaji fedha na limbikizo la riba katika madeni ya nje,” inasema sehemu ya ripoti hiyo ya BoT.


Ripoti hiyo inabainisha pia kuwa katika deni hilo, asilimia 76.6 ni deni la nje na asilimia 23.4 ni deni la ndani.


Ikifafanua, taarifa hiyo inasema kuwa deni la nje liliongezeka kwa asilimia 6.8 na kufikia dola za Marekani milioni 4,940.4. Katika kiasi hicho, dola milioni 4,010.2 zilikuwa ni deni halisi wakati dola milioni 1,268.2 sawa na asilimia 18.4 ya deni lote, lilitokana na malimbikizo ya riba.


Orodha ya taasisi za serikali zilizo madeni inaonyesha kuwa Serikali Kuu ndiyo inayoongoza kwa kuwa na deni linalofikia dola milioni 3,192.4 sawa na asilimia 79.6 ya deni lote ikifuatiwa na sekta binafsi ambayo inadaiwa dola milioni 647 (asilimia 16.1) na taasisi za umma zinadaiwa dola milioni 170.8 sawa na asilimia 4.3.


Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika mwezi huo, malipo ya madeni ya nje yalifikia dola milioni 3.8. kati ya kiasi hicho, dola milioni 2.2 zilikuwa malipo ya madeni halisi na dola milioni 1.6 zilikuwa ni malipo ya malimbikizo ya riba.


Kuhusu deni la ndani, ripoti hiyo inabainisha kuwa nalo liliongezeka na kufikia sh bilioni 1,885.3 ilipofika mwisho wa Oktoba, 2007 ikilinganishwa na deni la sh bilioni 1,860.8 lililorekodiwa mwezi mmoja kabla.


Katika kiasi hiki, dhamana za serikali zilikuwa ni asilimia 99.6 ya deni lote huku taarifa ikionyesha kuwa mabenki ya biashara ndiyo wakopeshaji wakubwa kwa serikali kwa kuikopesha asilimia 43.7 ya deni lote.


Kuhusu mfumko wa bei, taarifa hiyo inabainisha kuwa ulishuka na kufikia asilimia 7.1 mwezi Oktoba ikilinganishwa na asilimia 8.3 iliyorekodiwa mwezi Septemba.


“Kupungua kwa mfumko wa bei kunatokana na kushuka kwa mfumko wa bei ya vyakula kwa sababu mfumko wa bei ya vitu ambavyo si vyakula uliongezeka.


Katika kipimo cha mwezi, kiwango cha mfumko wa bei kilishuka na kufikia asilimia 0.4 kutoka asilimia 0.6 iliyorekodiwa Septemba.


Mfumko wa bei ya vyakula kwa kipimo cha mwaka ulishuka mwezi Oktoba na kufikia asilimia 8.4 kutoka asilimia 11.4 ilivyokuwa mwishoni mwa mwezi Septemba.


Katika kipindi cha Januari hadi Oktoba, wastani wa mfumko wa bei ulipungua kidogo na kufika asilimia 7 ikilinganisha na asilimia 7.1 iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita. Hali hiyo ilionekana pia katika wastani wa mfumko wa bei katika kipindi cha miezi 12.


Mfumko wa bei ya vitu ambavyo si chakula kwa kipindi cha mwaka uliongezeka na kufikia asilimia 5.1 mwishoni mwa Oktoba ikilinganishwa na asilimia 4.1 ya Septemba.


Hata hivyo, kwa kipindi cha kati ya Januari na Oktoba, wastani wa mfumko huo wa bei ulikuwa asilimia 7.2, kulinganisha na kiwango cha asilimia 7.9 kilichorekodiwa katika kipindi kama hicho cha mwaka uliotangulia.


Kwa upande a makusanyo ya kodi, ripoti hiyo inaonyesha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilivuka lengo la makusanyo kwa kukusanya sh bilioni 262.9 kulinganisha na lengo la kukusanya sh bilioni 254.2.


Taarifa hiyo ya BoT inaeleza kuwa mafanikio hayo yalitokana na TRA kuimarisha mbinu za kukusanya kodi na kufanya ukaguzi maalum katika sekta mbalimbali za kiuchumi ambazo zinalipa kodi nyingi.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents