Tragedy

Dereva wa waziri akatwa kichwa

KITENDAWILI cha mahali aliko Tumaini Mbaga, dereva wa Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohamed Aboud, aliyetoweka siku 10 zilizopita katika mazingira ya kutatanisha, kimeanza kuteguliwa baada ya mwili unaoaminika kuwa wa dereva huyo kukutwa ukiwa umetenganishwa kichwa na kiwiliwili.

na Schola Athanas

 

 

 

KITENDAWILI cha mahali aliko Tumaini Mbaga, dereva wa Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohamed Aboud, aliyetoweka siku 10 zilizopita katika mazingira ya kutatanisha, kimeanza kuteguliwa baada ya mwili unaoaminika kuwa wa dereva huyo kukutwa ukiwa umetenganishwa kichwa na kiwiliwili.

 

Mwili huo unaoaminika kuwa ni wa Mbaga kutokana na kiwiliwili kukutwa kikiwa na suruali inayofanana na ile aliyovaa dereva huyo mara mwisho alipoonekana Januari 19, mwaka huu, uligundulika ukiwa umeharibika kiasi cha kutotambulika.

 

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Pius Sheka, alisema kiwiliwili kinachoaminika kuwa ni cha marehemu huyo kilikutwa juzi Jumamosi katika eneo la Kwembe Kipera, njia panda ya barabara ya Kingazi, mpakani mwa Wilaya ya Kinondoni na Mkoa wa Pwani karibu na Makondeko.

 

Kwa mujibu wa Kamanda Sheka, baada ya kukutwa kwa kiwiliwili hicho, kichwa cha marehemu huyo kilichoonekana kutenganishwa kwa kuchinjwa kiligundulika siku moja baadaye, yaani juzi Jumapili, karibu kabisa na kilipokutwa kiwiliwili hicho.

 

“Maiti hiyo inayohisiwa kuwa ya dereva wa Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, ilipatikana Januari 26 (Jumamosi), saa 12 jioni katika eneo la Kwembe Kipera, kwenye barabara ya Kingazi, njia panda, ikiwa imeharibika vibaya kiasi cha kushindwa kutambulika huku ikiwa imetenganishwa kichwa na kiwiliwili,” alisema Sheka.

 

Alisema mwili ulikutwa ukiwa na suruali ya rangi ya kijivu marehemu aliyokuwa ameivaa alipopotea, huku ukiwa kifua wazi.

 

Kamanda Sheka aliwaambia wanahabari hao kuwa uchunguzi wa awali wa jeshi hilo ulionyesha kuwa marehemu aliuawa katika eneo tofauti na waliofanya kitendo hicho walikwenda kumtupa katika eneo ulipokutwa mwili wake.

 

“Uchunguzi wa awali katika eneo la tukio ulionyesha mwili wa marehemu ulitupwa katika eneo hilo baada ya kuuawa sehemu nyingine, kwa kuwa sehemu hiyo haikuonyesha kwamba kulikuwa na patashika yoyote,” alisema kaimu kamanda huyo.

 

Kamanda Sheka alisema polisi walipata taarifa za kuonekana kwa mwili huo kutoka kwa wananchi wanaoishi eneo hilo.

 

“Polisi walipofika eneo la tukio walikuta kiwiliwili kikiwa peke yake, lakini kwa kuwa ilikuwa ni jioni waliondoka bila ya kukiona kichwa. Siku iliyofuata (Jumapili) walirudi na kukuta kichwa kikiwa karibu na eneo la tukio,” alisema Sheka.

 

Kamanda Sheka alisema uchunguzi wa mwili wa marehemu unaendelea kufanywa na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na vielelezo kadhaa vimepelekwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi ikiwa ni pamoja na suruali ya marehemu. Maiti imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam.

 

Dereva huyu akiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser, lenye namba za usajili STK 2523, linalotumiwa na Naibu Waziri Aboud, alitoweka Januari 19, mwaka huu, mchana baada ya kumrudisha waziri huyo nyumbani kwake.

 

Kutoweka kwa dereva na gari hilo kuligunduliwa Januari 22 baada ya naibu waziri huyo kumsubiri dereva bila mafanikio.

 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, alikaririwa akisema dereva huyo alikuwa na mazoea ya kuegesha gari hilo katika ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kimara Temboni, Dar es Salaam, lakini siku hiyo hakufika eneo hilo.

 

Kwa mujibu wa Kamanda Tibaigana, taarifa za awali zilionyesha siku hiyo dereva huyo alimtumia mke wake ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS), akimpa taarifa kuwa amekwenda Dodoma kwa kuwa ameitwa na bosi wake ghafla.

 

Gari hilo lilionekana Januari 24, saa 10 jioni, likiwa limeegeshwa eneo la kuegesha magari, CCM, Tabata Kimanga, likiwa katika hali nzuri na lilionekana kuwa lilikuwa limeegeshwa siku ya pili yake, yaani Januari 23.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents