Diamond Platnumz

Diamond azidi kukamata roho za mashabiki wa Afrika Mashariki

Ulishashuhudia jinsi mashabiki hasa wa kike wanavyochanganyiwa wakiwaona mapacha wa P-Square wawapo jukwaani? Mbaya zaidi mzuka unapowapanda na kuamua kuvua mashati yao kuonesha vifua vyao vilivyojazia pamoja na yale matuta matatu tumboni yanayojijenga kutokanana mazoezi ya gym. Sehemu hizo kwa wanawake wengi huwachanganya kiasi cha kutamani kuwarukia na kuwakumbatia bila kujali jasho jingi linalowatiririka kutokana na makamuzi ya jukwaani. Infact wanasayansi wanasema jasho la mwanaume ling’aaro kwenye kifua cha mwanaume wa shoka huamsha hisia za kimapenzi kwa baadhi ya wanawake kama sio wote.

Wengine hufikia mpaka pointi ya kuduwaa utadhani wamemuona malaika mbele yao. Ama wengine huenda mbali zaidi mpaka kufikia kutokwa na machozi ya furaha kwa kuwaona tu wanamuziki hao. Mwanamuziki anapofikia kiwango hicho hayo ndio huitwa mafanikio.

Ni msanii gani hapa Tanzania mwenye uwezo wa kuwaliza mashabiki wake tena wale wa nchi zingine? Amini usiamini kwa sasa ni Diamond pekee ndiye mwenye uwezo huo. Umaarufu wa kijana huyu nje ya Tanzania unakuwa kwa kasi kuliko wengi wanavyodhani. Ndiye msanii aliyepo kwenye soko zaidi kuliko wengine wote wa Tanzania. Anatafutwa na mapromota mbalimbali ndani na nje ya nchi kama maji jangwani.

Imefikia wakati unaweza ukashindwa kumpata Diamond kwenye show yako kwasababu ana concert sehemu nyingine aliyolipwa zaidi. Jiulize kwanini hayupo kwenye Fiesta mwaka huu? Ni kwasababu ili waweze kumzungusha kwenye mikoa yote nchini, inabidi waweke bajeti kubwa ya kumlipa, ambayo inaweza kuwalipa wasanii zaidi ya kumi kwenye show moja. Kwa kauli yake mwenyewe hivi karibuni alisema show zake huanzia milioni 10 na kuendelea. Kawaida malipo ya show za Fiesta kwa kila msanii hayazidi shilingi milioni 1 kwa msanii mkubwa.

Weekend iliyopita Diamond alikuwa mjini Malindi nchini Kenya ambapo alipiga show ya kukata na shoka kwenye ukumbi wa Pata Pata Beach Club. Haikuwa show ya kitoto. Ni zile show ambayo wenzetu wa Marekani wanaziita ‘Sold out Concert’. Yaani zile show ambazo inabidi wakatishaji wa tiketi mlangoni waanze kuzuia watu kuingia sababu ndani pamejaa lasivyo watu watakanyagana.

Show ilifanyika kwenye eneo la kishua zaidi linaloashiria kuwa kiingilio kilikuwa kimechangamka, lakini mahudhurio yalionesha kama vile kiingilio kilikuwa bure.

Nyomi la kufa mtu!! Mashabiki wa kike walionesha kuchanganyikiwa na swagga za Diamond ambaye jina lake halisi ni Abdul Naseeb. Halafu kama vile alijua namna ya kuwashika mashabiki wa aina hiyo baada ya kuamua kuwa mhudhuriaji mzuri wa gym. Matokeo yake kama Peter na Paul Okoye, naye ameyatengeneza yale matuta matatu ya tumboni. Alipovua shati, wasichana waliokuwa mbele walitakaa kupaa na kwenda kupata kumbatio lake na kujisahau kuwa wengine wameongozana na wapenzi wao ambao ni wazi wangemind. Ama hakika Diamond aliacha gumzo mjini Malindi.

Kwa miaka mitano ijayo, huenda Diamond akawa msanii tajiri zaidi kuliko wote Tanzania. Haya mashavu anayoyapata si ya kawaida.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents