Habari

Dito shakani:Kufunguliwa kesi upya, mahabusu leo wagoma

Siku chache tu baada ya kuachiwa kwa dhamana na Korti Kuu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kapteni Mstaafu Ditopile Mzuzuri, yuko shakani kufunguliwa kesi nyingine mpya inayohusiana na ile inayomkabili sasa ya kumuua dereva wa daladala bila ya kukusudia.

Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Siku chache tu baada ya kuachiwa kwa dhamana na Korti Kuu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kapteni Mstaafu Ditopile Mzuzuri, yuko shakani kufunguliwa kesi nyingine mpya inayohusiana na ile inayomkabili sasa ya kumuua dereva wa daladala bila ya kukusudia.

Hofu juu ya kufunguliwa upya kwa kesi hiyo ambayo sasa ingali ikiendelea Kortri Kuu inatokana na tishio linalotolewa sasa na kiongozi wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, anayedai kuwa mkuu huyo wa zamani mkoani Tabora anastahili kushitakiwa kwa `Kesi ya Mauaji` na wala siyo ile inayoendelea sasa ya ‘kuua bila ya kukusudia`.

Akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu leo asubuhi, Mchungaji Mtikila amesema lazima afungue kesi hiyo mapema iwezekanavyo ili kuona haki ikitendeka, huku akidai kuwa ile ya sasa siyo hasa anayostahili kukabiliwa nayo Dito.

 

Akasema Mtikila kuwa leo atawasiliana na jopo la mawakili wake ili ikiwezekana, kama si mchana wa leo hii, kesho asubuhi aweze kuifikisha kesi hiyo mpya haraka iwezekanavyo.

 

`Mimi na wanaharakati wenzangu tumeamua kufungua kesi hii chini ya utaratibu wa mashtaka binafsi kwa sababu ya kutoridhishwa kwetu na namna kesi ya sasa ya Bw. Ditopile inavyoendeshwa,` akasema Mchungaji Mtikila.

 

Amesema hata kama mawakili wake watashindwa kutekeleza azma yake hiyo, yeye binafsi yuko tayari kutinga Mahakama Kuu, akidai kuwa anayo haki ya kikatiba kuweza kufanya hivyo.

 

`Mimi mwenyewe ni mwanasheria, na tena ni Mtanzania mwenye haki zote za kikatiba� ninayo haki ya kwenda mahakamani hata kama sitakuwa na wakili,` akasema, huku akiitaja Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ndiyo inayompa `jeuri` hiyo.

 

Amesema wakati akichukua uamuzi wa kwenda mahakamani kufungua kesi upya dhidi ya Dito, amemwandikia barua Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Alfred Tibaigana, akimtaka awalinde mashahidi muhimu waliokuwepo wakati wa tukio hilo.

 

Katika kesi ya sasa, Ditopilie ambaye aliachiwa kwa dhamana na Korti Kuu, anadaiwa kuwa mnamo Novemba 4 mwaka jana, mishale ya saa 1:00 usiku, katika barabara ya Bagamoyo na Kawe, jijini Dar es Salaam, alimuua bila ya dereva wa daladala Hassan Mbonde kwa kumpiga risasi.

 

Wakati huohuo, kitimtim cha aina yake kimeibuka leo katika Mahakama ya Kisutu Jijini baada ya mahabusu kugoma wakitaka nao kesi zao ziendeshwe haraka kama ilivyo kesi ya Ditopile.

 

Kazi zote za mahakama hiyo zimesimama kuanzia saa 2 :00 asubuhi baada ya kuwasili kwa makarandinga yaliyobeba mahabusu, ambapo mahabusu hao waligoma kutelemka kwenye malori hayo.

 

Mahabusu hao wamegoma kutelemka kwenye malori mawili yenye namba za usajili STH 3058 na STJ 903 yaliyowaleta mahakamani hapo wakihoji kuwa inakuwaje upelelezi wa kesi inayomkabili Ditopile umewahi kukamilika na kuziacha kesi za walalahoi ambao wanaendelea kusota rumande kwa miaka kadhaa sasa.

 

Kufuatia mgomo huo, eneo zima la Mahakama ya Kisutu lilijaa askari kanzu, askari wa kawaida na wale wa kikosi cha kutuliza ghasia, FFU, ambao walimwagwa kwa wingi.

 

Hali hiyo imemlazimu Hakimu Mkuu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Bw. Sivangilwa Mwangesi kutoka nje ya mahakama kujaribu kuwashawishi mahabusu hao watelemke kwenye gari ili mahakama iendelee na shughuli zake.

 

Hata hivyo hakuna mahabusu aliyemsikiliza na badala yake, mahabusu hao waliendelea kushusha nyimbo za mapambio ya kilokole, wakitaka nao wahakikishiwe kuwa kesi zao zitasikilizwa haraka kama Dito.

 

Mpaka Gazeti hili linakwenda mitamboni, mambo yalikuwa bado mabichi kwenye viwanja vya mahakama ya Kisutu na askari wakaamua kuwarejesha mahabusu hao gerezani.

 

Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents