Ditopile afariki dunia

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kapteni mstaafu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri (60) amefariki dunia katika Hoteli ya Hilux, iliyopo mkoani Morogoro

Ditopile Mzuzuri


 


Ashton Balaigwa na Venance George, Morogoro


ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kapteni mstaafu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri (60) amefariki dunia katika Hoteli ya Hilux, iliyopo mkoani Morogoro.

Ditopile alifariki dunia ghafla jana alfajiri kwenye hoteli hiyo akiwa pamoja na mke wake mdogo, aliyefahamika kwa jina moja la Tabia, wakati akifuatilia taarifa mbalimbali kwenye runinga.

Kifo cha Ditopile kimethibitishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Meshack Massi ambaye alisema kuwa, marehemu alifariki kabla ya kufikishwa katika hospitali hiyo.

Akielezea tukio hilo, Dk Massi alisema kuwa, walipata taarifa za kuugua ghafla kwa Ditopile akiwa hotelini hapo, na kutuma wauguzi kwenda kutoa huduma ya kitabibu kabla ya kumkimbiza hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa mganga huyo baada ya matabibu hao kufika katika hoteli hiyo walibaini kuwa, ameshafariki na kwamba, mpaka sasa bado wanachunguza sababu za kifo chake.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya hoteli hiyo zinaeleza kuwa, marehemu akiwa pamoja na mke wake mdogo aliyefahamika kwa jina la Tabia, walifika hotelini hapo Aprili 18 majira ya saa 5:00 usiku wakitokea jijini Dar es Salaam na kupanga chumba namba 106 katika hoteli hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, marehemu akiwa pamoja na mkewe na mdogo wake aliyefahamika kwa jina la Selemani Mzuzuri, aliyekuwa akimuendesha marehemu kwa kutumia gari aina ya Nissan, walitoka asubuhi ya Aprili 19 na kurejea majira kati ya saa 5:00 na saa 6:00 usiku.

Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa, majira ya saa 3:00 asubuhi ya jana mke wa marehemu alitoa taarifa kwa uongozi wa hoteli hiyo akijulisha kuwa, hali ya mumewe ni mbaya na kwamba, alikuwa akihitaji msaada wa kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Uongozi wa hoteli hiyo ulifika chumbani kwa marehemu na kumkuta akiwa amelala sakafuni huku akiwa hajitambui, wakatoa taarifa kwa mdogo wa marehemu na Jeshi la Polisi, ambao walifika pamoja na waganga kisha walimchukua na kumkimbiza hospitalini kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.

Hata hivyo, baadaye waganga walibaini kuwa, alikuwa amefariki dunia akiwa hotelini.

Baada ya kubainika kuwa alikwishafariki, uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali Mkoa wa Morogoro waliamua kuwa, mwili wa wamerehemu uhifadhiwe katika chumba cha maiti katika hospitali hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye alisema taarifa ya Mganga Mkuu wa Mkoa ilisema, Ditopile alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini.

Alifahamisha kuwa, marehemu alifika mkoani Morogoro kwa shughuli zake binafsi, ambapo siku moja kabla ya kifo chake akiwa na mkewe pamoja na mdogo wake, walikwenda kukagua mashamba yake yaliyoko eneo la Mgongola, wilayani Mvomero na kurudi mjini Morogoro majira ya saa 3:00 usiku.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, marehemu pamoja na wenzake waliamua kutorejea jijini Dar es Salaam kutokana na muda kuwa mbaya kusafiri, mvua na uchovu waliokuwa nao, kisha wakaenda kuwatembelea ndugu zao mjini hapa na kurudi hoteli kwenye saa 5:00 usiku.

Alisema majira ya alfajiri marehemu akiwa na mkewe aliamka akiwa na afya njema na kusali sala ya alfajiri na kisha wakaanza kuangalia vipindi vya runinga na ndipo mauti yalipomkuta, mkewe akiwa amepitiwa na usingizi.

Kamanda Andengenye alisema kuwa, baada ya mkewe kuamka alikuta mumewe akiwa taabani na kushindwa kupumua na kuamua kutoa taarifa kwa ndugu zake pamoja na uongozi wa hoteli hiyo.

Umati mkubwa wa wakazi wa mjini Morogoro wakiwemo viongozi wa chama na serikali walimiminika katika hospitali ya mkoa, kufuatia kifo hicho cha ghafla cha mwanasiasa huyo mkongwe na kiongozi wa muda mrefu wa CCM na serikali kabla ya kujiuzulu kutokana na tuhuma za kuua pasipo kukusudia.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo alisema amesikitishwa na kifo cha Ditopile na kueleza kwamba, mbali ya kufahamu kama aliwahi kuwa mkuu wa mkoa, lakini pia alikuwa ni mdogo wake na waliwahi kuishi pamoja jijini Dar es Salaam .

Naye Katibu wa CCM mkoani hapa, Mary Chatanda alisema chama chake kimesikitishwa na kifo cha Ditopile, ambaye alikuwa mwanachama na kada wao mwaminifu.

Hata hivyo, mdogo wa marehemu Selemani Mzuzuri aliyekuwa akimuendesha marehemu mpaka mwisho wa uhai wake, alishindwa kuzungumzia tukio la kifo cha kaka yake kutokana na kugubikwa na simanzi kwa kufiwa na kaka yake.

�Naelewa waandishi wa habari mnahitaji kupata taarifa, lakini siwezi kuzungumzia tukio hili, limenichanganya sana,� alisema huku akibubujikwa machozi.

Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Yusuf Makamba alifika mjini hapa kutokea Dodoma baada ya kupata taarifa ya kifo hicho, na kueleza kuwa amesikitishwa sana na kifo hicho na kwamba, yeye binafsi anamfahamu vema marehemu.

Alisema licha ya kuwa kada mzuri wa CCM pia aliwahi kufanya naye kazi serikalini na jeshini.

Mwili wa marehemu Ditopile Mzuzuri, ulitarajiwa kuhamishiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, jana jijini Dar es Salaam kutoka katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Naye Festo Polea toka Dar es Salaam anaripoti kuwa, mwili wa marehemu Ditopile Mzuzuri unatarajiwa kupokelewa nyumbani kwake maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam, leo saa 4:00 asubuhi ukitokea Hospitali ya Lugalo.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani hapo, mdogo wa marehemu, Abdallah Mwinshehe Ditopile alifahamisha kuwa, mwili wa marehemu baada ya kupokelewa na kuagwa na ndugu na marafiki, saa 7:00 mchana utapelekwa katika Msikiti wa Tambaza, kwa ajili ya kusomewa dua na Kaimu Mufti, Abubakar Zuber na mazishi yatafanyika saa 9:00 jioni katika makaburi ya kifamilia yaliyopo Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Abdallah alisema kaka yake aliondoka jijini Dar es Salaam, kuelekea mkoani Morogoro, Ijumaa alfajiri akiwa mzima wa afya njema hadi mauti yalipomkuta akiwa na mkewe.

Abdallah alisema kifo cha Ditopile kinaweza kikawa kimesababishwa na BP ya kushuka, iliyokuwa ikimsumbua kwa muda mrefu na kwamba pia alikuwa anasumbuliwa na kisukari tangu mwaka 1995.


 


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents