Habari

Dk Mwele amwagiwa pongezi baada ya kupata shavu WHO

Salamu za pongezi zimeendelea kumiminika kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika vya Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.

Pia, Dk Mwele aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mpango wa Maalumu wa WHO wa kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele (Espen) na sasa atahamia kituo chake cha kazi Congo-Brazaville. Mradi wa Espen ulianza kutekelezwa mwaka 2016 hadi 2020 na una lengo la kumaliza magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwa kutoa vifaa tiba, elimu na dawa.

Miongoni mwa waliomtumia pongezi ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Sikika, Irenei Kiria ambaye aliandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Hongera Mwele kwa kupata nafasi hiyo ina maana ulipangwa kulisaidia Taifa letu ukiwa nje.”

Mwingine ni Mhadhiri wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo aliyeandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema: “Nina furaha kwa uteuzi wa Dk Mwele kuwa Mkurugenzi wa WHO. Nahisi kusamehewa kwa kuikosoa Serikali baada ya kumuondoa NIMR.”

Dk Mwele aliondolewa kuwa Mkurugenzi wa NIMR na Rais John Magufuli Disemba 16 mwaka jana. Kuondolewa kwake katika nafasi hiyo kulifanyika siku moja baada ya kutoa ripoti ya utafiti wa magonjwa, ndani yake ikiwamo taarifa ya virusi vya ugonjwa wa Zika katika maeneo ya Morogoro, Geita na Magharibi mwa Tanzania.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents