Dk. Mwinyi atilia mkazo Teknohama

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amesema Tanzania haiwezi kubakia kisiwa katika suala la maendeleo ya teknolojia, hivyo ametoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa maendeleo ya teknolojia yanapewa kipaumbele

na Mkolo Kimenya




WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amesema Tanzania haiwezi kubakia kisiwa katika suala la maendeleo ya teknolojia, hivyo ametoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa maendeleo ya teknolojia yanapewa kipaumbele.

Akizungumza jana katika uzinduzi wa Wiki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dk. Mwinyi alisema Tanzania inatakiwa kuimarisha sekta hiyo kutokana na ukweli kwamba ndiyo nyenzo muhimu inayotumika kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya uchumi wa dunia katika karne hii.

Dk. Mwinyi alisema ili kuweza kutumia kikamilifu fursa ya TEKNOHAMA katika kujiletea maendeleo, inahitajika mikakati ya makusudi ya kuwaandaa wananchi kwa kuwapa elimu bila ubaguzi.

“Kila mwananchi bila kujali anakaa kijijini au mjini, wasomi au si wasomi, ni lazima waandaliwe kutumia fursa za TEKNOHAMA kwa kuondoa mgawanyiko uliopo katika matumizi, ili kukuza uchumi ikiwa ni pamoja kwenda sambamba na karne ya sayansi na teknolojia,” alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, aliwataka watoa huduma za mawasiliano kulitafutia ufumbuzi tatizo la mahitaji maalumu ya watu wenye ulemavu kwa kuweka mikakati ya kitaifa kwa kuhimiza utengenezaji wa vifaa vya teknolojia ambavyo vitatoa huduma muafaka kwa mahitaji yao.

“Haina maana yoyote ya kuwa na teknolojia kibao wakati hakuna watu wa kuzitumia, hivyo ni lazima kujali makundi yote, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha na kuwahamasisha zaidi,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), John Mkoma, alisema hivi sasa wapo katika mchakato wa kuunganisha mfumo utakaokuwa na uwezo mkubwa wa kuwasiliana kwa zaidi ya nchi nane za Afrika.

Alisema mfumo huo ujulikanao ‘ICT backbone’ umeshaunganishwa katika baadhi ya mikoa ya hapa nchini na kwamba utaanza kufanya kazi wakati wowote, hivyo kurahisisha mawasiliano hata kwa watu waishio vijijini.

“Mpango huu ni wa nchi nane za Afrika lakini kwa upande wa Tanzania tumeanza kuutengeneza katika baadhi ya mikoa ambayo mawasiliano yake yalikuwa si mazuri na utaanza kutumika muda si mrefu kuanzia sasa,” alisema na kuongeza kuwa unategemea kugharimu dola za Marekani milioni 170 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwaka 2010.



Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents