Habari

Dk. Slaa atisha mtu kwa bastola

MBUNGE wa Karatu, Dk. Willbrod Slaa (CHADEMA), ameingia katika mzozo na mtu aliye na mgogoro naye kuhusu shamba, baada ya jana kumtishia kwa bastola.

na Tamali Vullu

 

MBUNGE wa Karatu, Dk. Willbrod Slaa (CHADEMA), ameingia katika mzozo na mtu aliye na mgogoro naye kuhusu shamba, baada ya jana kumtishia kwa bastola. Dk. Slaa mwenyewe alilithibitishia gazeti hili kuwa alilazimika kuchomoa bastola yake na kupiga risasi hewani kwa lengo la kumtisha kijana huyo, mkulima mmoja wa Karatu, katika ugomvi wa shamba.

 

Katika tukio hilo, Dk. Slaa, alisema kuwa alifyatua risasi moja hewani kwa lengo la kuzima tafrani iliyoanzishwa na mkulima huyo, Daniel Yanffan Areso.

 

Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu kutoka Karatu, Dk. Slaa, alikiri kufyatua risasi hiyo baada ya kijana huyo kumvamia yeye na watoto wake walipokuwa wanalima shambani humo kwa kutumia trekta.

 

Alisema akiwa shambani na watoto wake, mkulima huyo alifika shambani hapo akiwa na fimbo na kuanza kumchapa dereva wa trekta hilo.

 

“Kutokana na hali hiyo, vijana wangu waliingilia kati, lakini nilipoona ugomvi umekuwa mkubwa, nilifyatua risasi hewani ili kumtisha kijana huyo,” alisema Dk. Slaa.

 

Alisema baada ya muda polisi walifika kwenye eneo hilo na kuchukua maelezo yake kuhusu tukio hilo.

 

Dk. Slaa alisema anashangazwa na kitendo cha mkulima huyo kudai shamba hilo ni lake, kwani yeye alilinunua mwaka 1999.

 

Alisema kutokana na tukio hilo, polisi wamemshauri kufungua kesi ya jinai dhidi ya mkulima huyo kutokana na kumvamia katika eneo lake na kumfanyia vurugu.

 

Naye Areso akielezea tukio hilo, alisema Oktoba mwaka huu alipanda maharage na mahindi katika shamba hilo, lakini alishangazwa na kitendo cha mbunge huyo kwenda kulima shambani kwake.

 

Alisema jana alipofika shambani hapo, alianza kumzuia dereva wa trekta asiendelee kulima, ndipo watoto wa Dk. Slaa walimvamia na kuanza kumpiga sehemu mbalimbali mwilini.

 

Areso alisema katika tukio hilo, Dk. Slaa alitaka kumuua kwa kumfyatulia risasi, ambayo kwa bahati nzuri ilimkosa.

 

“Nilipoona hivyo, nilikimbia na kwenda kutoa taarifa polisi ambao walifika eneo la tukio na kumchukua Dk. Slaa na kumpekea kituoni.

 

“Katika maelezo yake, polisi alieleza kuwa alifyatua risasi hewani, lakini alifyatua akinilenga kutaka kuniua na bahati nzuri ilinikosa,” alisema.

 

Areso, alisema kutokana na tukio hilo amefungua jalada namba KRP/RB3032/2007 linalohusu shambulio.

 

Alisema kutokana na kupigwa fimbo sehemu mbalimbali mwilini, anahisi maumivu makali na amekwenda zahanati ya serikali ilyopo jirani ambako amepatiwa matibabu.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents