Dola 400 kuteketeza kemikali chakavu

ZAIDI ya dola 400 za Marekani zitatumika kuteketeza kila tani moja ya kemikali chakavu zilizokusanywa nchini, kazi itakayofanyika nchini Ujerumani. Ofisa Kilimo Mkuu wa Wizara ya Chakula na Kilimo, Dk. Francisca Katagile, aliyasema hayo hivi karibuni kwenye mkutano wa siku mbili wa tathimini ya mradi wa viatilifu na umasikini ulioandaliwa na shirika linalojishughulisha na mazingira la AGENDA.

na Nasra Abdallah


ZAIDI ya dola 400 za Marekani zitatumika kuteketeza kila tani moja ya kemikali chakavu zilizokusanywa nchini, kazi itakayofanyika nchini Ujerumani. Ofisa Kilimo Mkuu wa Wizara ya Chakula na Kilimo, Dk. Francisca Katagile, aliyasema hayo hivi karibuni kwenye mkutano wa siku mbili wa tathimini ya mradi wa viatilifu na umasikini ulioandaliwa na shirika linalojishughulisha na mazingira la AGENDA.


Alisema mpaka sasa tani 1,200 tayari zimeshakusanywa katika maghala 350 na kinachosubiriwa ni upatikanaji wa makontena ya kuweza kusafirisha kemikali hizo, ambapo kwa sasa zabuni zimeshatangazwa.


Alisema mradi huo umechukua muda mrefu kutokana na kemikali hizo kutakiwa kusafirishwa kwa uangalifu, ili zisije kuharibu mazingira.


Aidha, Dk. Katagila, alisema bado jamii haina uelewa kuhusu kemikali hatari zaidi ya zile zinazoua papo kwa hapo na kusahau zile zinazochukua muda mrefu katika mwili ambapo madhara yake huonekana baadaye.


Mbali na jamii alisema pia baadhi ya wahudumu wa afya hawajui dalili za mtu aliyeathirika na kemikali, jambo linalosababisha mgonjwa akifikishwa hospitalini kuanza kupatiwa matibabu tofauti na ugonjwa.


Hata hivyo, alisema serikali haina budi kuwa mwangalifu katika utumiaji wa kemikali hizo kama vile DDT, kwani zinachangia katika uharibifu wa mazingira na kuangamiza viumbe hai.


Kwa upande wake, Ofisa Mipango wa Shirika la AGENDA, Bashiru Abdi, alisema jumla ya asasi zisizo za kiraia 30 zimepatiwa mafunzo na shirika hilo jinsi ya kuweza kuepuka matumizi ya kemikali chakavu lengo likiwa kuzijengea uelewa, ili nao waende kuifundisha jamii.


Abdi alisema kuendelea kutumika kwa kemikali hizo miongoni mwa jamii kumetokana na mamlaka husika kutokuwa na tabia ya kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa jamii, ili ipate kujua ni dawa zipi zinafaa na zipi hazifai na nini athari zake.


Mradi wa utekelezaji wa kemikali chakavu, umehusisha nchi saba za Afrika, ikiwemo Ethiopia, Afrika Kusini, Nigeria, Mali, Tunisia, Moroco na Tanzania.


Jumla ya sh bilioni 6.9 zimetolewa na mashirika mbalimbali ya Ulaya katika kutekeleza mradi huo, likiwemo Shirika la Global Facility, Serikali ya Uholanzi, Umoja wa Nchi za Ulaya na Global Environment Facility.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents