Habari

DR Congo, Mgombea wa upinzani, Martin Fayulu adai kwenda kupinga ushindi wa Rais Felix Tshisekedi mahakamani

Mgombea wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) uliofanyika Disemba 30 ameapa kuyapinga matokeo mahakamani. Martin Fayulu ameiambia BBC kuwa raia wa Congo wanastahili kujua ukweli wa uchaguzi, mabao ameutaja kuwa ni “mapinduzi”.

Kwa mujibu wa BB, Mgombea mwengine wa upinzani Felix Tshisekedi, alitangazwa kuibuka na ushindi katika kinyang’anyiro hicho, lakini kumekuwa na tuhuma kuwa mshindi huyo ameingia makubaliano ya kisiasa na rais aondokaye Joseph Kabila.

Tayari watu kadha wanaripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa toka matokeo hayo yalipotangazwa.

Uchaguzi huo unakamilisha safari ya miaka 18 madarakani ya Joseph Kabila.

Matokeo hayo, endapo yatathibitishwa, yataweka historia ya makabidhiano ya amani ya hatamu za uongozi toka nchi hiyo ilipopata uhuru wake toka kwa wakoloni wa Ubelgiji mwaka 1960.

Kanisa lenye ushawishi mkubwa la Katoliki ambalo lilikuwa na waangalizi wa uchaguzi 40,000 limesema matokeo yaliyotangazwa hayaendani na matokeo waliyonayo.

Fayulu amesema nini?

Akiongea na mhariri wa BBC wa Afrika Fergal Keane, Bw Fayulu amesema atayapinga matokeo hayo kwenye mahakama ya katiba.


“Nitafanya kila liwezekanalo kwangu kufanya ukweli udhihiri sababu Wacongo wanataka mabadiliko,” amesema.

Fayulu hata hivyo ameweka wazi kuwa kuna uwezekano mdogo wa kushinda kesi hiyo sababu mahakama “imeundwa na watu wa Kabila” lakini amesema hataki kuwapa kisingizio wapinzani wake kuwa hakufuata sheria.

“Felix Tshisekedi ameteuliwa na Kabila ili kutekeleza matakwa ya utawala wa Kabila. Kabila ndiye bosi,” amedai Fayulu.

“Kabila hawezi kubaki na kusuka mpango na mtu ambaye hatakuwa na mamlaka yeyote… Tshisekedi anajijua kwamba hakushinda uchaguzi.”

Fayulu amesema ana hofu kuwa kutatokea vurumai kama tume ya uchaguzi (Ceni) haitatoa takwimu sahihi za “kituo kimoja kimoja cha kupigia kura” na kusisitiza kuwa ni haki ya kila Mkongomani kuandamana kwa mujibu wa sheria.

Maelfu ya mashabiki wa Tshisekedi wameingia mitaani kwa furaha kusherehekea ushindi walioupata, lakini upande wa pili wafuasi wa Fayulu wamejitokeza mitaani kupinga matokeo hayo.

Matukio ya ghasia yameripotiwa katika eneo la Kikwit, ambapo polisi wawili na raia wawili wanasemakana kuuawa.

Kuna ripoti pia mamia ya wanafunzi wamekuwa wakipinga matokeo hayo kwa kuandamana na kutimuliwa na mabomu ya machozi katika mji wa Mbandaka.

Maandamano pia yameripotiwa katika eneo la Kisangani, lakini kusini ambapo Tshisekedi anaungwa mkono kwa wingi kumekuwa na sherehe.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amezitaka pande zote kujizuia kufanya ghasia.

  • Felix Tshisekedi 7,051,013 (38.57%)
  • Martin Fayulu Madidi 6,366,732 (34.83%)
  • Emmanuel Shadary 4,357,359 (23.84%)

*Waliojitokeza kupiga kura wanakisiwa ni 48%.

Wagombea wenye dukuduku na matokeo wanatakiwa kuwasilisha hoja zao mahakamani saa 48 toka kutangazwa kwa matokeo ya awali.

Majaji itawachukua siku saba kupitia kesi na kutoa maamuzi.

Mtaalamu wa masuala ya Katiba Jacques Ndjoli ameiambia BBC kuwa kuna matokeo ya aina tatu ambayo yanayotarajiwa : mosi mahakama inaweza kuthibitisha ushindi wa Tshisekedi, pili kuamuru kura zihesabiwe upya na tatu kufuta matokeo yote na kuamuru kura zipigwe upya.

Mahakama ya katiba haijawahi kubatilisha matokeo kabla, na wengi wanawaona majaji wake kuwa washirika wakubwa wa chama tawala.

Iwapo ushindi wa Tshisekedi utathibitishwa basi ataapishwa ndani ya siku 10.

Tshisekedi ameusifu ushindi wake na kuahidi kuwa “raisi wa Wakongomani wote”.

Msemaji wake Louis d’Or Ngalamulume amekanusha vikali uwepo wa makubaliano yoyote na Kabila.

Chama tawala cha Kabila ambacho kimeshika nafasi ya tatu hakijayapinga matokeo hayo.

Nje ya Congo kumekuwa na mchanganyiko wa maoni ya kutaka watu kuwa watulivu na wengine wakitaka ufafanuzi wa kilichotokea.

Mkuu wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat amesema: “Ni muhimu kwa mtanziko wowote wa matokeo, hususani kuwa hayajaakisi matakwa ya wananchi, inabidi utatuliwe kwa njia ya amani kwa kutumia sheria na makubaliano ya kisiasa kwa pande zinazohusika.”

Uchaguzi DRC

Marekani imewasifu wapiga kura kwa kuwaita mashujaa na kutaka maswali yote tata kuhusu kura na matokeo yapatiwe majibu sahihi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters ameomba kuwepo na ufafanuzi kuhusu matokeo hayo akisema ushindi wa Bw Tshisekedi unaenda kinyume na uhalisia mashinani.

“Kanisa Katoliki la Congo lilifanya hesabu yake na kutoa matokeo tofauti kabisa,” amenukuliwa na shirika hilo.

Nchi ya Ubelgiji ambayo iliitawala DRC wakati wa ukoloni imeungana na Ufaransa katika kutilia mashaka matokeo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje Didier Reynders amenukuliwa la shirika la habari la Reuters akiiambia redio ya taifa RTBF kuwa Ubelgiji itatumia nafasi yake ya muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka taarifa rasmi ya kilichotokea.”Tuna mashaka na inabidi tuhakikishe na kujadiliana suala hili katika vikao vya Baraza la Usalama,” Bw Reynders ameongeza.

By Ally Juma


Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents