Habari

Eric Mutta: Mtaalam wa computer aliyeshinda ruzuku (grant) ya shilingi milioni 500 (Exclusive)

Ukipewa kitita cha shilingi milioni 500 utakifanyia nini? Eric Mutta ambaye hivi karibuni kupitia uwezo wake wa hali ya juu katika fani ya utengenezaji software za computer alijishindia ruzuku (grant) ya dola 328,232 anaweza akawa na jibu sahihi.

eric-on-mics-2
Eric Mutta

Fedha hizo kutoka kwa taasisi ya Financial Sector Deepening Trust (FSDT) ilimuendea Eric na kampuni yake ya Problem Solved Limited.

me-sos-handshake
Eric akikabidhiwa check yake na FSDT kwenye hafla iliyofanyika katia hoteli ya Serena (Movenpick)

Kampuni yake iliyashinda makampuni mengine 13 makubwa ya kifedha kwa ugunduzi wake alioupa jina ‘Minishop’.

Tofauti na vijana wengi wa Kitanzania, Eric alianza kufahamu masuala ya computer akiwa na umri wa miaka 14 tu.

“Baba alinunua computer used (yani haikua mpya), akatuachia mie na wadogo zangu tuwe tunacheza game moja inaitwa Prince of Persia. Baada ya kumaliza game nilianza kuchunguza vitu vingine kwenye computer na mwisho wake nikagundua fani ya programming,” anasema Eric.

parents-me-smile
Eric akiwa na wazazi wake

Hapo ndipo alipogundua masuala ya computer ni kipaji chake na hivyo kuamua kusomea fani hiyo.

Mafanikio hayakumwendea kirahisi. Baada ya kuajiriwa kwa kipindi cha miezi sita, aliamua kuacha kazi na kuamua kuwa mjasiriamali na mwaka 2008 alifanikiwa kuanzisha mtandao wa kijamii uliojulikana kama Tuwasiliane.

“Mtandao ulikua na kufikisha wanachama zaidi ya elfu 10 walioenea kwenye kila mkoa nchini Tanzania,” anasema.

Hata hivyo licha ya kuwa na wanachama wengi kiasi hicho, mambo yalimwendea mrama.

“Nilijikuta nakosa kipato cha maana wakati gharama ziko juu (mtandao ulikua unatuma zaidi ya SMS 1,000 kwa siku na ni enzi zile kabla ya mambo haya ya SMS za bure). Kampuni ilifilisika nikalazimika kurudi kwenye ajira, ila nilijua huko mbele nitarudi na mzuka mpya kabisa kwahiyo sikuifunga.”

Akiwa na malengo ya kutatua baadhi ya vitendawili vinavyoumiza watu wengi kwenye masuala ya computer na taasisi za kifedha, 25 April 2008 Eric alianzisha kampuni yake, Problem Solved kwaajili ya kutatua matatizo sugu kwa kutengeneza computer software.

Mwezi huu taasisi ya Financial Sector Deepening Trust (FSDT) ilimtangaza Eric na kampuni yake kama washindi wa kitita cha shilingi milioni 500.

“Walivyotangaza kwamba mie mshindi, kwanza nilipata amani maana niliumiza kichwa sana, na vile vile nikapata imani kwamba hamna kitu nisichoweza kufanya nikiweka nguvu zangu zote. Nilipata kujiamini kiasi hichi kwasababu nilishapata mafanikio mwaka 2012 nilivyo shinda millioni 24 kutoka kwa US Department of State,” anasema.

Eric amesema kupitia fedha hizo ataajiri watu hadi 7 ili wamsaidie na kazi ya kufikisha Minishop system kwa biashara zaidi ya 130,000 nchini. Pia anasema atatanunua laptops 500 za kuuza zikiwa na hiyo system ndani.

“Kuna mradi wa kuanzisha training kwa vijana wa kidato cha nne kwenye fani ya kuendesha biashara za maduka. Mwisho kuna zoezi la kujenga mtandao wa ma agent wakusambaza hiyo Minishop system, na vile vile kukusanya malipo kwa wateja.”

Ili kijana aweze kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio, Eric anasema ni lazima azingatie masuala matatu.

“Kwanza awe na uthubutu wa kuwaza vitu ambavyo wenzake wanaweza kumuita kichaa wakisikia anaviongea. Ni ile jeuri ya kuwaza kununua ndege siku moja wakati leo hii mtu unapanda baiskeli,” anasema.

“Pili awe mtu wa kuchapa kazi, na asipende wala kukubali vitu vya bure. Kama wenzake wanafanya kazi masaa matano, basi yeye afanye masaa mia tano. Alipie kila anachoomba, na adai malipo kwa kila anachopewa akielewa kwamba muda wake unathamani na si wakuchezea.

Tatu asimsahau Mungu na wazazi wake, maana hapo ndo atakapopata muongozo mzuri wa kumlinda na vishawishi vya maisha ambavyo siku zote hufilisi watu kimya kimya. Vijana wakiendelea kula bata kila Jumamosi tutakua tunawazika kila Jumapili.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents