Habari

Esther Wasira: ‘Hakuna chama chenye haki miliki ya nchi ya Tanzania’ (mdahalo wa Nyerere Day)

Esther Wasira akitoa hoja kwenye mdahalo

Mwanaharakati kijana na mwanasheria nchini, Esther Wasira amesema hakuna chama chenye haki miliki ya nchi ya Tanzania na kwamba amani imejengwa na wazee akiwemo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Bi. Wasira amesema hayo leo (Oct.14) kwenye mdahalo maalum uliondaliwa na JUMUIYA ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) wa kumuenzi hayati Baba wa Taifa uliofanyika kwenye ukumbi wa Nkrumah katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, UDSM.

Amesema amani itaendelea kubaki nchini kama tu tutadumisha haki na usawa.

“Nimewahi kusikia maneno haya, ‘mabadiliko yakitokea katika nchi bwana unajua yataleta vita maendeleo tutakosa’ mimi kwakweli I’m saying hii ni completely wrong notion,” alisema Bi.Wasira.

“Mwalimu Nyerere alisema kwamba, amani ni sawa na mti, na mti wowote mpaka ustawi unahitaji upaliliwe, unahitaji uwekewe mbolea, unahitaji uwekewe maji. Na akasema kwamba mbolea hiyo na maji hayo ni haki na usawa katika nchi yoyote. Tukifanikiwa basi kuviweka hivi tutakuwa tumepalilia mti wetu wa amani. Na hivyo haki na usawa ni vipi? Fikiria haki ya elimu, haki ya kupata kazi, haki ya kutotofautiana kipato, sanasana tena wenye kipato wenyewe hatujui hata kama wanalipa kodi au hata wamezipata kwenye njia gani za rushwa kuiibia serikali, hiyo sio haki. Sasa mimi najiuliza, hawa watawala wa sasa wamefanikiwaje na kwa kiasi gani kuupalilia mti wa amani?

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba amesema ili watanzania tuweze kumuenzi vema Baba wa Taifa ni muhimu kuzingatia elimu ambayo ndio mkombozi.

Amesema elimu inayotakiwa kusisitizwa ni ile inayoweza kumfanya mtu awe na uwezo wa kuchanganua mambo na kuleta mabadiliko katika jamii na sio elimu yenye lengo la kupata kazi peke yake.

“Wasomi wangapi wamemaliza hayo mashahada ya uzamili na uzamivu ni mabingwa wa kutisha wa kuweza kutengeneza matofali ya kuchoma? Wako wangapi hapa wasomi wanaoweza kusaidia kijiji kiondokane na nyumba ya matope na nyumba ya miti lakini kikaweza kujenga angalau nyumba ya matofali ya kuchoma?”amesema.

“Mwalimu amebeba matofali, wengi hapa mnaona aibu kushika tope, mwalimu ni mtu wa ajabu, huko alikolala na alale pema.”

Miongoni mwa wachangiaji wengine kwenye mdahalo huo alikuwa ni meya wa Ilala mheshimiwa Jerry Silaa na mhadhiri wa UDSM Bi. Vicensia Shule.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents