Habari

EU yasema Tanzania ina haki kutosaini mkataba wa EPA

Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Roeland Van de Geer amesema Tanzania ina haki ya kuamua kutosaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara na Jumuiya ya Ulaya (EPA) hadi itakapojiridhisha manufaa yake.

dsc_0007

Alitoa kauli hiyo Alhamisi hii jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu masuala mbalimbali pamoja na kujibu maswali ya wanahabari hao.

Akizungumzia suala la Tanzania kutosaini mkataba huo wa EPA, ambao nchi wanachama waliosaini hufanya biashara bila kutoza kodi, Balozi Van de Geer alisema ingawa wasiwasi wa Tanzania kuwa mkataba huo utadhoofisha juhudi za nchi za kufufua viwanda vyake, haoni kama kuna ushindani kwenye hilo.

“Ingawa sioni ushindani unaohofiwa na Tanzania kwenye soko la EPA, lakini uamuzi wake wa kutosaini ni haki yao na nisisitize kuwa ni vyema Tanzania isisaini mkataba wowote ambao wana mashaka nao hadi pale watakapojiridhisha umuhimu wake,” alisema Balozi Van de Geer.

“Ni vyema nchi ikachukua muda kujiridhisha badala ya kukimbilia kusaini, kwa sababu endapo baadaye wataona mkataba huo hauna manufaa na huku wameusaini, watasononeka hivyo ni vyema wakaupitia na kuona kama una maslahi kwao,” aliongeza.

Awali, Septemba mwaka huu, Mwenyekiti wa EAC, Rais John Magufuli alisema viongozi wote kwa pamoja walikubaliana kupewa muda wa miezi mitatu ili Sekretarieti ya EAC iangalie na kupitia masharti ya EPA kabla ya kusaini ili kila mmoja afaidike.

Hata hivyo, katika jumuiya hiyo ya EAC, nchi ambazo tayari zimesaini mkataba huo ni Kenya, Rwanda na Uganda na nchi zilizobaki ni Tanzania na Burundi. Rais Magufuli alisema katika kikao hicho, walibaini mambo 10 ambayo yanapaswa kuangaliwa kabla ya kufikia uamuzi kwa maslahi ya nchi na wananchi.

BY: EMMY MWAIPOPO

CHANZO: HABARI LEO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents