Bongo5 Exclusives

Exclusive: Kilichomkuta msanii Loon baada ya kusilimu

Je umewahi kufuatilia na kujua msanii Chauncey Hawkins ambaye wengi wanamjua zaidi kama Loon baada ya kutoka ukristo na kuhamia dini ya kiislamu miaka kadhaa iliyopita anaitwa nani? na kwa sasa anafanya nini? Ama yuko wapi?

Well, msanii huyo aliwahi kuwika katikati ya miaka ya tisini akiwa ni mmoja wa memba wa kundi la Bad Boy kama msanii, mtunzi na mwandishi wa wasanii wa kundi hilo, na pia kuwahi kuja Tanzania August mwaka 2006.

Bongo5 imepata nafasi ya kulonga na meneja wake ambaye pia alikuja naye hapa Tanzania na kuelezea exclusively nini kinaendelea na msanii huyo. Na hii ni update ya kinachoendelea juu yake.

Akiwasiliana moja kwa moja na mmoja wa mapaparazi wetu meneja wa zamani wa msanii huyo kutoka gazerezani amesema kwa sasa Loon anajulikana kama Amir Junaid Muhadith na kwamba aliamua kusilimu bila kulazimishwa baada ya kufikiria sana namna maisha yake yalivyokuwa yanakwenda.

Amesema nia ama wazo la kusilimu alilipata wakati akiwa ametembelea Dubai na kushangaa watu wote wakiacha kila kitu walichokuwa wanafanya na kukimbilia msikitini ambapo yeye aliisikia sauti nzuri iliyokuwa ikisikika kupitia vipaza vya sauti mbali mbali vilivyokuwa karibu kila pembe ya mji huo.

Anasema jambo hilo lilimshtua sana kiasi cha kushangaa inakuwaje mji ambao una kila kitu kama wafanya biashara wakubwa, majengo mazuri na kila aina ya utajiri inapoita adhana basi kila kitu kinasimama kupisha swalaa halafu baada ya hapo watu wanarudi na kuendelea na mambo yao.

Aliendelea kusema kitu hicho kilimfanya kufikiria mara mbili mbili akikumbuka alipotoka ambapo yeye binafsi aliamini kuna mafanikio makubwa ya kiuchumi, siasa, utajiri, viwanda, ulinzi n.k akimaanisha Marekani.

Cha kushangaza tofauti iliyopo baina ya hizi nchi mbili ni kwamba Marekani pamoja na kuwa na wakristu wengi hakuna watu wanaoacha shughuli zao kama mikutano ya kibiashara, siasa kwa ajili dini yao kama alivyoshuhudia plae Dubai. Jambo lile lilimfanya aanze kufuatilia kwa undani kuhusu Uislamu, na muktadha wake.

Aidha, meneja huyo anasema Loon alipata upinzani mkubwa sana kutoka kwenye familia yake ambayo haikuridhia yeye kubadili dini na pia hata baada ya kubadili din, baadhi ya taasisi za ki usalama Marekani zilianza kumchunguza pamoja na kuzuia passpoti yake mara kadhaa ili asisafiri kwenda ghuba ya uajemi ambapo ndipo wanaona palipokuwa kichocheo kikubwa kwa yeye kusilimu na pia kwamba alikuwa wanajaribu kuangalia kama anao uwezo wa kuwashawishi wamarekani vijana na kufuata njia yake.

“Hivi ninavyoongea na wewe yupo ndani, ana kesi ambayo bado ipo mahakamani na kwa sasa yupo ( gerezani) tangu mwezi wa tano ambayo ilianzia Novemba mwaka jana baada ya yeye kwenda Ulaya nchini Belgium katika mhadhara na ndipo vyombo vya usalama vikamfungulia mashtaka yanayohusiana na kusafirisha ama kuuza unga unaotokana na safari zake za mara kwa mara nje ya Marekani mwaka 2006 hadi 2008,”alisema Meneja huyo.

Meneja anaendelea kuchonga kwamba wanausalama wa Marekani walisababisha akashikiliwa huko huko Belgium Novemba 22 na kuzuia akaunti pamoja na mali zake zote, kabla ya kusafirishwa na kurudishwa Marekani mwezi wanne mwaka huu ambapo yupo katika gereza la New Hanover County Detention Center hadi sasa.

Akizungumza na mdau wetu meneja huyo alisema kabla ya kuswekwa ndani na kufunguliwa mashtaka Amir (Loon), alikuwa anafanya kazi ya mahubiri ya Quran katika maeneo mbali mbali nchini Marekani na hata kimataifa katika nchi nyingine kama ilivyokuwa Belgium, ambapo ndipo alipokamatwa.

Msanii Loon alitembelea Tanzania mwaka 2006 na kufanya kolabo na Ibra Da Hustler ambaye alikuwa ni mmoja wa kundi la Nako 2 Nako Soulders pamoja na msanii mwenzake D Gritty kutoka Marekani.

Kesi yake itaendelea kusikilizwa Mwezi Desemba baada ya kusogezwa mbele kutoka mwezi huu wa kumi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents