Afya

FAHAMU: Dalili 10 za mwanzo za mtoto anayefanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono

Kwa sasa kumekuwa matukio kadha wa kadha yanayohusu unyanyasaji kingono, ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo hususani wa shule za Chekechea, Msingi hadi Sekondari.

Je, utajuaje kama mtoto wako anafanyiwa vitendo hivyo viovu pindi anapoenda shuleni? jambo la kwanza na msingi ni vyema ukajenga utamaduni wa kumkagua mtoto wako kila siku jioni au usiku muda wa kulala.

Wataalamu wengi wa masuala Saikolojioa ya malezi wanasema kuwa, mzazi ni vyema ukawa karibu zaidi na mtoto wako ili umsome baadhi ya tabia mpya pia umfanye awe huru kueleza jambo lolote pindi anapopatwa na tatizo.

Kumbuka pia kabla ya kuzifahamu dalili za mtoto anayefanyiwa vitendo hivi viovu, ni vyema ukajua kwamba hili ni tatizo kubwa kwenye jamii zetu na sio jukumu la serikali tu bali ni jukumu la kila mtu hivyo, kwa pamoja tukemee vitendo hivi.

Hizi ndio dalili 10 za mwanzo ambazo mtoto anayenyanyaswa kingono huwa anazionesha mara nyingi.

  1. Mtoto anapata shida wakati wa kukaa au kutembea. (Dalili hizi ni kuanzia watoto wa miaka Miwili hadi 10)
  2. Anaogopa kupita kiasi baadhi ya watu, mahali au vitu. (Hii ni kuanzia mwaka mmoja hadi mitano)
  3. Anapenda kujishika sehemu za siri mara kwa mara na hali hii humtokea hadi usiku akiwa amelala.
  4. Anakaa chooni muda mrefu au kuhitaji kujisaidia mara kwa mara. (Hii huwatokea watoto wenye umri kuanzia mwaka 1-5)
  5. Usiku anapatwa na malue malue au anaweweseka usiku. (miaka 1-5)
  6. Anakataa/kusumbua kula na muda mwingine kutapika bila ugonjwa. (Miaka 0-5)
  7. Analia sana. (Miaka 0-3 )
  8. Anaona aibu na kujitenga. (umri wote 0-17)
  9. Anashindwa kuzuia haja kubwa. (Umri kati ya miaka 4-7)
  10. Anakuwa mkimya isivyo kawaida (Umri wa balehe).

Hizo ni dalili 10 za mwanzo lakini kuna dalili nyingine kama

  1. Anashuka kielimu. (Miaka 6-17)
  2. Anakuwa na kiburi, maamuzi ya kukinzana na maagizo. (Umri wa balehe)
  3. Mimba (Miaka 11-17)
  4. Majaribio ya kujiua. (Miaka 8- 17)
  5. Anakimbia nyumbani mara kwa mara (Miaka 8-17)
  6. Anakataa kushiriki shughuli za nyumbani, za shule, za kiroho. (7-17)

Dalili hizi ni kwa msaada wa Shirika la Sema Tanzania, hata hivyo hizi ni dalili tu mojawapo kwani zipo nyingi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents