Michezo

Fahamu sababu zilizopelekea rekodi ya Kipchoge ya kukimbia km 42 kwa saa 1:59 kutotambuliwa kimataifa

Fahamu sababu zilizopelekea rekodi ya Kipchoge ya kukimbia km 42 kwa saa 1:59 kutotambuliwa kimataifa

Mkenya Eliud Kipchoge ameweka jina lake katika vitabu vya historia , akimaliza kilomita 42 za mbio za marathon kwa saa moja dakika 59 na sekunde 40 katika shindano la Ineos siku ya Jumamosi nchini Austria Vienna.

Hatahivyo muda huo bora uliowekwa na bingwa huyo hautatambulika kama rekodi ya dunia.

Kulingana Shirika la Riadha duniani IAAF , kwa mbio yoyote kufikia sheria zake na hivyobasi kutambulika kama rekodi ya dunia kuna masharti yanayopaswa kufuatwa kulingana na chombo cha habari cha AFP.

  • 1.Kwanza mbio hizo lazima ziwe zimeandaliwa na shirika la riadha duniani IAAF ama shirikisho la raidha la nchini ambapo riadha hizo zinaandaliwa.
  • 2.Wanariadha wanaodhibiti kasi hawawezi kuingia katika mbio hizo kwa zamu na kutoka.
  • 3.Lazima wanariadha wafanyiwe vipimo vya matumizi ya dawa za kusisimua mwili
  • 4. Vinywaji vinapaswa kutoka kwa vituo rasmi na sio kupewa mwanariadha na wasimamizi wake.
  • 5. Ni Sharti kuwepo zaidi ya washindani watatu katika mbio hizo.
  • 6. Mwanariadha hafai kudhibitiwa kasi na gari lililopo mbele yake.
  • 7. Njia itakayotumika ni sharti ifanyiwe ukaguzi na kupimwa na maafisa wa IAAF.

Wakati wa jaribio la kwanza la mbio hizo za marathoni huko Monza nchini Itali miaka miwili iliopita, Kipchoge alipatiwa vinywaji huku wadhibiti mbio hizo wakibadilishwa mara kwa mara, hatua iliokiuka masharti ya IAAF.

Siku ya Jumamosi , alipewa vinywaji kila baada ya kilomita 5 na hivyobasi kukiuka sheria hizo za shirikisho la riadha duniani.

Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 34 tayari anashikilia rekodi ya dunia miongoni mwa wanaume katika umbali huo akiwa na muda wa saa mbili dakika moja na sekunde 39, ambao aliweka katika mbio za Berlin tarehe 16 mwezi Septemba 2018.

Kulingana na AFP , barabara hiyo ilikuwa imeandaliwa hali ya kwamba ingemchukua Kipchoge sekunde 4.5 zaidi kulingana na uchanganuzi wa wataalam wa michezo katika chuo kikuu cha Vienna.

Kwa jumla aliweza kushuka mita 26 na kupanda mita 12 , walisema wataalam hao.

Mbio hizo za marathon zimekuwa na ushindani mkali katika kipindi cha miaka 16 iliopita kati ya wanariadha wa Kenya na wenzao wa Ethiopia.

Mataifa hayo mawili ni washindani wakuu wa mbio ndefu uwanjani.

Rekodi ya Kipchoge ilikaribia kuvunjwa na raia Muethiopia Kenenisa Bekele ambaye alikimbia saa 2 dakika moja na sekunde 41 ikiwa ni sekunde mbili pekee kabla ya kuivunja rekodi hiyo.

Mbio hizo za Viena hazikuwa mashindano bali zililenga kuwapa motisha mamilioni ya watu duniani. Na Kipchoge amefanikiwa.

Katika mahaojiano na vyombo vya habari , Kipchoge alisema kwamba mbio hizo za Vienna zililenga kuwapatia changamoto wanadamu katika maisha yao ya kila siku.

Pia aliwashutumu wakosoaji wake.

Ninakimbia kuweka historia , ili kuuza #NoHumanLimited na kuwapa motosha zaidi ya watu bilioni 3 . Sio swala la fedha bali kubadilisha maisha ya watu”, alinukuliwa akisema.

Chanzo BBC

By Ally Juma.

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents