Siasa

FFU yasambaratisha wananchi Bagamoyo

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakiwa na silaha jana walilazimika kuzuia maandamano ya wananchi zaidi ya 2,000 waliokuwa wamepania kurudi kwenye shamba la Matunda Estate lililopo katika kijiji cha Pengwa, kata ya Zinga, wilaya ya Bagomoyo, mkoani Pwani.

Na Lucy Lyatuu

 
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakiwa na silaha jana walilazimika kuzuia maandamano ya wananchi zaidi ya 2,000 waliokuwa wamepania kurudi kwenye shamba la Matunda Estate lililopo katika kijiji cha Pengwa, kata ya Zinga, wilaya ya Bagomoyo, mkoani Pwani.

 

Wananchi hao walipigwa marufuku mwaka jana na serikali, kutovamia shamba hilo kwa kuwa linamilikiwa `kihalali` na Matunda Estate.

 

Tamko la kuwataka wananchi hao kutovamia shamba hilo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 4,500, lilitolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Rita Mlaki, Oktoba 20, mwaka jana.

 

Wananchi hao walikuwa wakiandamana wakiwa na mabango yaliyosomeka `DCI upelelezi miaka mingapi juu ya Matunda Estate?`-`Mashamba ni ya kwetu, anatumwa polisi na ardhi wapi na wapi`-`Hatujafahamu azma

 

Inatoka Uk.1
ya mkuu wa mkoa ya kutaka kutudhulumu`, na lingine lilisomeka: `Tunataka mashamba yetu, Waziri Mkuu ndiye mkombozi`.

 

Hata hivyo, maandamano hayo hayakusababisha vurugu za aina yoyote zaidi ya kuwepo na majibizano makali kati yao na FFU wakitaka waruhusiwe kuingia katika mashamba kwa ajili ya kuangalia mazao yao.

 

Akizungumza na wananchi hao jana, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Aron Kissanga, alisema ametumwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Pwani, kuzuia maandamano yao na kuwataka wananchi hao kufuatilia suala hilo kwa amani katika ngazi husika.

 

`Kamanda amenituma niwaombe muondoke kwa amani, ili muweze kufuatilia suala lenu katika ngazi husika, na kwa utaratibu utakaoeleweka,` alisema Bw. Kissanga.

 

Alisema Mkuu wa wilaya ameahidi kukutana na wananchi hao Aprili mosi, ili kuzungumzia madai yao.

 

Wananchi hao waliondoka eneo hilo kwa amani baada ya kusikiliza ujumbe kutoka kwa Bw. Kissanga, na kumuomba kupeleka taarifa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. John Magufuli wakitaka ahudhurie siku hiyo.

 

Hatua ya wananchi hao ilitokana na madai kuwa shamba hilo si la Matunda Estate.

 

Mwenyekiti wa wananchi hao, Bw. Deo Mwankemwa, alisema wamesuburi zaidi ya miezi sita tangu serikali itoe amri hiyo lakini sasa wamechoka na kwamba watarudi katika shamba hilo kwa ajili ya kuangalia mazao yao.

 

Alisema baada ya serikali kutoa amri hiyo mwaka jana, walifuatilia kwa kina ili kufahamu Matunda Estate ni nani na kwamba ana mamlaka gani kwa kuwa hajaendeleza kiwanja hicho tangu mwaka 1999.

 

`Tulikwenda hadi kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BREILA) na kubaini kuwa hakuna jina kama hilo,` alisema Bw. Deo.

 

Aliongeza kuwa, waliendelea kufuatilia kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. John Magufuli na kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Mizengo Pinda bila mafanikio.

 

Aidha, alisema baada ya kutopata ukweli wa jambo linaloendelea, wameamua kurudi katika shamba hilo ili kuvuna baadhi ya mazao yao waliyokuwa wakilima.

 

`Licha ya kwamba kuna askari zaidi ya watano wanaolinda shamba hilo wakiwa na silaha, sisi tutaingia rasmi kwa ajili ya kuendelea na shughuli zetu za kilimo, kwani hatuwezi kufa njaa wakati mazao yapo mashambani,` alisisitiza mwananchi mwingine, Bi. Fatma Mwina.

 

Alimuomba Rais Jakaya Kikwete kutofumbia macho suala hilo kwani wananchi hao kwa pamoja wameamua kufa au kupona kwa ajili ya kupata mashamba yao.

 

`Ndani ya mashamba hayo, tumelima mihogo, karanga, nazi, matikiti maji na mazao mengine, halafu tunaambiwa eti tuyaache wakati huo watoto nyumbani hawana chakula tunabaki omba omba!`

 

Alipohojiwa kwa simu kabla ya tukio la jana, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Christine Ishengoma alisema amepata taarifa za kurudi kwa wananchi hao katika shamba hilo.

 

Hata hivyo, Dk. Ishengoma alisema ofisi yake haina uwezo wa kulizungumzia kwa kina suala hilo kwa kuwa kwa sasa halipo mezani kwake.

 

`Suala hilo halipo katika mikono yangu tena, tayari lipo wizarani, hivyo ni jukumu la viongozi husika kulizungumzia,` alisema Dk. Ishengoma.

 

Na Nipashe ilipofika katika ofisi za Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Rita Mlaki, Katibu Muhtasi wake alisema yuko nje ya nchi kwa ziara ya kikazi.

 
Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents