Habari

Gavana wa Nairobi Sonko amekanusha madai yanayomkabili ya ufisadi, kukaa mahabusu mpaka tarehe hii – Video

Gavana wa Nairobi Sonko amekanusha madai yanayomkabili ya ufisadi, kukaa mahabusu mpaka tarehe hii - Video

Mahakama jijini Nairobi imeamuru Gavana wa Nairobi Mike Sonko kusalia mahabusu hadi siku ya Jumatano (tarehe 11) wakati ombi lake la dhamana litakapoamuliwa.

Hakimu mkuu wa mahakama ya kupambana na ufisadi Douglas Ogoti akitoa uamuzi huo, pia amemwamrisha Inspekta Jenerali wa Polisi kuwakamata na kuwawasilisha washukiwa wengine waliotajwa na idara ya mkuu wa mashtaka ya umma waliokosa kufika kortini hii leo.

Mawakili wa Sonko walikuwa wamewasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana, wakisema kwamba mteja wao anaumwa na anahitaji matibabu ya kina. Hata hivyo, upande wa mashtaka umepinga ombi hilo na kusema kwamba kutaepusha uwezekano wa mashahidi kutishiwa, kuingiliwa kwa kesi na pia kufanya hivyo, ni hatari kwa sababu tayari mtuhumiwa anasemekana kuwa na historia ya kukimbia jela.

”Kuhusu kuzuiliwa haswa kuhusu mshatakiwa wa kwanza na baada ya kusikiliza pande zote kuhusu maswala mengine yote.Ninatoa amri kama ifuatavyo. Ninamwamrisha Inspekta Jenerali wa Polisi kuwakamata na kuwawasilisha mahakamani washukiwa wote ambao hawakufika hii leo koti hii itakapoketi tena”.

”Korti hii itatoa uamuzi wake siku ya Jumatano ya tarehe 11 mwezi huu. Washtakiwa watazidi kuzuiliwa.Kutokana na mshukiwa wa kwanza kuhitaji matibabu ya dharura licha ya kuwa kuna pingamishi,ninaamrisha apelekwe hospitali baada ya kituo cha matibabu cha idara ya magereza kuhakikisha akiwa na daktari wake ili kumwezesha kupelekewa kwenye hospitali nyingine yoyote punde hilo litapopangwa.” Douglas Ogoti, Hakimu, Mahakama ya kupambana na Ufusadi.

SonkoHaki miliki ya pichaMIKE SONKO/TWITTER

Gavana na wenzake watashikiliwa katika gereza la Industrial Area. Hii ni baada ya upande wa mashtaka kusema kwamba shirika la kupambana na ufisadi kukiri kutokuwa na nafasi ya kutosha ya kuwashikilia watuhumiwa wote.

Vilevile, upande wa mashtaka ulitoa maagizo ya kumzuia Sonko na maafisa wengine wa umma kufika katika ifisi zao za utendaji kazi hadi kesi hiyo itakaposikilizwa.

Aidha, wametaka watuhumiwa kupigwa marufuku ya kuwasiliana,kutishia mashahidi au wachunguzi pamoja na kuwasilisha paspoti zao mahakamani.

Mashtaka ni yapi?

Gavana wa Nairobi Mike Sonko ameshtakiwa katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi na makosa kadha yanayohusiana na kutolewa kwa zabuni ya zaidi ya dola 3.5 za Marekani.

Akiwa mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya ufisadi Douglas Ogoti, Sonko alishatkiwa pamoja na maafisa wengine wanane wa serikali ya jimbo wanaoaminika kujinufaisha kutokana na zabuni hizo.

Gavana huyo na wenzake walishtakiwa na makosa tofauti ya ufisadi kama vile kupanga kufanya kitendo cha ufisadi, kukosa kufuata sheria ya manunuzi serikalini, kutumia vibaya mamlaka za ofisi zao pamoja na kutwaa mali ya Umma kinyume na sheria.

Pia walishtakiwa kwa udanganyifu na kupokea fedha zinazotokana na ufisadi.

Wote wamepinga mashtaka dhidi yao.

Upande wa Mashtaka wapinga kuachiliwa kwa Sonko kwa dhamana

Upande wa mashtaka umepinga Gavana Sonko kuachiliwa kwa dhamama ila haujapinga maombi ya dhamana ya washtakiwa wengine.

Mawakili wa Gavana huyo hata hivyo wanaitaka koti kumwachilia huru wakidai aliumizwa wakati wa kukamatwa kwake eneo la Voi na maafisa wa polisi na hivyo anahitaji matibabu zaidi.

Hakimu Mkuu Chacha Ogoti anatarajiwa kutoa uamuzi huo hii leo.

Hatma ya Kaunti ya Nairobi

Kwa sasa kaunti ya Nairobi haina naibu gavana jambo ambalo limezua gumzo kali. Kulingana na katiba ya kenya iwapo gavana hawezi kufanyakazi na naibu wake pia hawezi kufanya kazi vilevile, spika wa bunge la kaunti atashikilia kwa siku 60, katika tukio hili akiwa ni Beatrice Elachi. Hayo ni kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisheria Alutalala Mukwahana.

Na katiba hiyo hiyo inasema baada ya siku 60 wananchi warudi debeni. Lakini kulingana na Bwana Mukwahana, walioandaa katiba hawakutarajia kwamba hili litatokea ilihali Gavana mwenyewe bado yupo.

Je sokomoko hii inaweza kutatuliwa vipi?

Katiba inamruhusu Rais Kenyatta kuvunjilia mbali serikali yoyote ya kaunti iwapo mazingira ya kipekee yatatokea na kufanya utendakazi wa serikali hiyo uwe mgumu.

Mtazamo wa mchambuzi wa masuala ya kisheria Alutalala Mukwahana iwapo atakosa kuungwa mkono na magavana wengine kuna uwezekano wa rais kuivunja serikali ya Sonko na kuiweka Nairobi katika serikali kuu.

Alutalala Mukwahana anafafanua kwamba katika Kamati ya maridhiano maarufu kama BBI, kuna pendekezo kuwa Nairobi ivunjiliwe mbali. ”Mwaka 1975 hayati Kenyatta alikubaliana na Umoja wa Mataifa kwamba makao makuu ya Umoja huo yatakuwa Kenya na wakaweka masharti baina yao na serikali kuu kwamba hali ya miundo mbinu na utendakazi wote katika jiji utakuwa ni wenye kuhakikisha makao hayo makuu utakuwa ni wenyewe kuendesha shughuli zake bila kusumbuliwa.”

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents