Habari

HakiElimu yaifumua bajeti ya elimu nchini

SIKU moja baada ya wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuitaka serikali ichukue hatua kali dhidi ya HakiElimu, taasisi hiyo imeibuka na kusema fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya elimu nchini hazitumiki ipasavyo.

na Ratifa Baranyikwa na Shabani Matutu


SIKU moja baada ya wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuitaka serikali ichukue hatua kali dhidi ya HakiElimu, taasisi hiyo imeibuka na kusema fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya elimu nchini hazitumiki ipasavyo.


Hayo yamo katika uchambuzi uliofanywa na taasisi hiyo kwa kuangalia mwenendo mzima wa bajeti na matumizi yaliyotengwa katika mwaka wa fedha 2006/07 uliomalizika hivi karibuni.


Ikitumia takwimu rasmi za serikali, HakiElimu imechapisha vijarida maalumu vinavyoonyesha mapungufu hayo katika sekta ya elimu ambavyo vilizunduliwa jijini Dar es Salaam, juzi.


Vijarida hivyo vinaainisha mchakato mzima wa bajeti ya elimu, hasa kwa upande wa ruzuku maalumu kwa wanafunzi wa elimu ya msingi.


Kwa mujibu wa vijarida hivyo, wakati ambapo bajeti iliyopitishwa na Bunge kwa mwaka huo ilikuwa sh bilioni 178, matumizi halisi yalikuwa sh bilioni 103 sawa na asilimia 58 ya fedha yote iliyoidhinishwa.


Kijarida cha uchanganuzi wa matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kinaeleza kuwa, fedha nyingi zilizoidhinishwa na Bunge, zinazofikia sh bilioni 75, hazikutumika na kwamba mtazamo wa karibu unaonyesha kuwa, sh bil. 14.6 ziliidhinishwa kwa ajili ya ruzuku maalumu kwa kila mwanafunzi, lakini hakuna fedha zilizotengwa au kutumika.


Taarifa iliyotolewa na HakiElimu na kusainiwa na Mkurugenzi wa shirika hilo, Rakesh Rajan, inaeleza pia kwamba, mbali ya hayo, vipaumbele vilivyoainishwa wakati wa bajeti ya mwaka jana bungeni, havikuzingatiwa.


Akitoa mfano, Rajan alisema kuwa, ruzuku maalumu (capitation grant) kwa wanafunzi wa elimu ya msingi, ilipangwa iwe sh 12,500, lakini kiasi kamili hakifiki mashuleni kwa wakati.


Taarifa hiyo inazidi kueleza kuwa, uzoefu unaonyesha kuwa shule zimekuwa zikipokea kiwango cha chini ya kile kilichopitishwa katika bajeti na kwamba kwa mwaka 2005/06 fedha nyingi hazikutumika ipasavyo, kinyume na bajeti iliyopitishwa na Bunge.


Kwa mujibu wa kijarida hicho, sh bilioni 12.4 ziliidhinishwa kwa ajili ya shule, lakini hakuna fedha zilizotengwa au kutumika.


Hata hivyo, imebainika kuwa, mishahara na gharama za shule viliendelea kuwa kipaumbele, lakini masurufu, mkutano, ukarimu na safari ambavyo vilipewa asilimia nane ya matumizi ya bajeti, vilichukua sehemu kubwa zaidi ya bajeti.


Kwa mujibu wa uchambuzi wa HakiElimu, maeneo mengine yaliyovuka matumizi ni pamoja na ofisi, huduma na ukarabati vitu ambavyo vinaelezwa kuwa si vipaumbele kwa kuboresha elimu kwenye ngazi ya jamii.


Aidha, kwa upande wa matumizi ya bajeti ya chakula, yalizidi kwa zaidi ya sh bilioni moja, kitu ambacho kimeelezwa kuwa ni cha kushangaza kwa kuzingatia upungufu wa nusu ya kiasi kilichoidhinishwa kilitumika kwenye chakula cha shule.


Kutokana na hali hiyo, HakiElimu imetoa changamoto kwa Wizara ya Elimu kuhakikisha inaandaa bajeti inayotoa vipaumbele bora kwa mambo yatakayoboresha ubora wa elimu kwenye kiwango cha shule, pia kuhakikisha matumizi yake halisi yanarandana na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.


Taasisi hiyo inashauri kuwa, masuala kama vile ruzuku maalumu kwa kila mwanafunzi, itolewe kama ilivyopangwa kwani ni muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia shuleni.


Taasisi hiyo imeitaka pia wizara kuangalia namna ya kupunguza matumizi ambayo si muhimu kwa ngazi za shule, kama vile masurufu kwa wafanyakazi wa wizara.


Hata hivyo, taasisi hiyo imeipongeza serikali kwa kuongeza fedha katika bajeti ya elimu kwa mwaka huu, lakini ikasema kuwa, kuongeza bajeti peke yake haitoshi.


Imeishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuzingatia vipaumbele vya MMEM na MMES, hasa suala la ruzuku maalum kwa kila mwanafunzi kwa kuwa ndiyo fedha muhimu inayotumika kununua vifaa vya kujifunzia na kufundishia.


Wakati huo huo, watu kadhaa waliohojiwa na gazeti hili, wamepingana na msimamo wa wabunge wawili wa CCM walioitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya matangazo yanayotolewa na HakiElimu.


Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti jana jijini Dar es Salaam, wananchi hao wameitaka serikali isiwasikilize wabunge hao na badala yake iache HakiElimu itimize wajibu wake wa kuikumbusha pale palipo na mabonde ili wapasawazishwe.


Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mtakatifu Anthony, Luis Ibrahimu, alisema kwamba si kweli kwamba matangazo hayo yanaweza yakazuia juhudi za maendeleo.


“Sikubaliani na kauli hiyo, ila mimi kama mwalimu, ninachoamini ni kwamba matangazo ya HakiElimu yanasaidia kuionyesha serikali yetu mahali ambako panakuwa na upungufu na wao kuparekebisha,” alisema Ibrahimu.


Aliendelea kusema kuwa, HakiElimu walitakiwa kupewa ushirikiano kutokana na michango yao katika kuhakikisha kuwa sehemu ambazo zimesahaulika zinakumbukwa.


Naye Kassimu Idrisa alisema kwamba si kweli kwamba matangazo haya yanaleta chuki kati ya serikali na wananchi wake, ila yamekuwa na lengo la kuionyesha serikali kasoro zilizopo katika sekta ya elimu.


“Kama kweli serikali ingekuwa imefanya juhudi kubwa za kuendeleza elimu, sidhani kama matangazo haya yangekuwa yanawashtua kiasi hiki, isitoshe mara baada ya kuingia madarakani serikali ya awamu ya nne iliomba kukosolewa pale inapokosea,” alisema Idrisa.


Aliongeza kuwa, anaamini serikali ya awamu ya nne haitachukua uamuzi kama huo kwa kuwa inaamini mchango wa asasi hiyo kama changamoto kwao, isipokuwa wanaoitaka ifungiwe ndiyo wasiotakia mema maendeleo ya elimu.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents