Hali Inasikitisha

Hali Inasikitisha
Asilimia 18 ya watoto 1,400 waliopimwa afya zao mwaka jana katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) iliyopo Mwanza, wamegundulika
kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Profesa Jumanne Maghembe amesema asilimia 30 ya Watanzania
hawajui kusoma na kuandika. Je tutafika kweli??

Kadhalika, baadhi ya watoto hao wameonekana kupata maambukizo hayo kutoka kwa mama zao wakati wa kunyonyeshwa huku wengine wakiwa wamepata maambukizi hayo wakati wa kuzaliwa.

Hayo yalibainishwa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Bugando, Dk. Charles Majinge, alipokuwa akitoa taarifa kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa kliniki ya watoto wanaoishi na VVU hospitalini hapo.

Aidha, Dk. Majinge alisema idadi ya vifo vya watoto huenda ikapanda maradufu hadi kufikia asilimia 50 na watoto watakaoathirika katika kukumbwa na vifo hivyo ni wale walio na umri wa chini ya miaka miwili, na kwamba jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa na wadau wote wa afya ndani ya mkoa, taifa na nje ya nchi, ili kuondokana na kuepusha maafa hayo ya watoto wadogo.

Naye Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa Mwakyusa, alisema ujenzi wa kituo hicho umekuja wakati mwafaka na kwamba serikali itajitahidi kuisaidia vifaa na mambo mengine katika kliniki hiyo, ili iweze kutoa huduma nzuri zaidi. Kujengwa na kukamilika kwa kliniki hiyo itapunguza idadi ya vifo vya watoto hasa walio na umri wa chini ya miaka miwili.

Katika hafla nyingine Profesa Maghembe alisema “Asilimia 30 ya Watanzania wote hawajui kusoma wala kuandika, hii inatufanya tuendelee kupambana, lakini hatuwezi kuwafanya wajue kusoma kama hakuna vitabu, tutafanya kila namna kuhakikisha vitabu vingi vinachapishwa ili watu wapate vitabu vya kujifunzia,” alisema.

Alisema serikali haina mpango wa kufuta kitabu chochote kinachotumika shuleni kwa sasa, ila inataka kuongeza idadi ya vitabu ili kufanya wanafunzi wawe na tabia ya kujisomea zaidi.

Aidha, alisema kati ya watoto wote wa wafugaji, asilimia 97.5 wameweza kwenda shule, lakini asilimia 2.5, hawajakwenda kutokana na kukosa watu wa kuwasukuma, ili waende shule.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents