Habari

Hali ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa Msumbiji, Umoja wa Mataifa waeleza

Msemaji wa Umoja wa mataifa amesema kuwa hali ya Kaskazini mwa Msumbiji ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa, hii ni baada ya siku chache kimbunga Kenneth kutuwa nchini humo.

 

Kimbunga hicho kilituwa siku ya Alhamisi kwa upepo mkali wenye kasi ya 220km/h (140mph) kilichoviangamiza vijiji.

Takriban watu 700,000 sasa wanadhaniwa kuwa katika hatari katika eneo hilo wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha.

Pemba, mji mkubwa wa jimbo la Cabo Delgado kumeshuhudiwa mvua yenye kina cha mita mbili na mafuriko.

Msemaji katika ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinaadamu (Ocha) Saviano Abreu ameeleza kwamba hali ni mbaya katika miji ya Macomia na Quissanga, akiongeza kwamba kuna wasiwasi pia kwa kisiwa kisichoweza kufikiwa cha Ibo.

Mawimbi ya hadi mita 4 yanatarajiwa, na mashirika ya misaada yanahofia kwamba mvua itazidi kunyesha.

“Tuna wasiwasi mkubwa kwasababu, kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, mvua nzito inatarajiwa kunyesha katika siku nne zijazo,” Deborah Nguyen, msemaji wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa , alieliambia shirika la habari la AFP.

“Tunatarajia mvua iwe na ukubwa wa mara mbili zaidi ya ilioshuhudiwa wakati wa kimbunga Idai,” ameongeza.

Kimbunga Idai kilisababisha vifo vya watu 900 katika nchi tatu mnamo Machi mwaka huu.

Inadhaniwa kwamba watu 400,000 wanaishi Pemba, na mvua kubwa imesababisha watu wengi kuwa katika hatari.

Kuna wasiwasi unaotokana na maporomoko ya ardhi katika mtaa wa Mahate mjini humo, maafisa wa Ocha katika eneo hilo wanasema, na katika mtaa wa Natite, nyumba zimeanza kuporomoka.

Shirika la mpango wa chakula duniani limetakiwa kuanza kutoa misaada kwa watu waliokwama, lakini barabara zilizoharibika zimesababisha shughuli zisitishwe katika maeneo yaliotengwa sana.

Takriban watu watano wamefariki kutokana na kimbunga hicho na takriban nyumba 35000 zimeharibika vibaya au kubomoka kabisa, maafisa wa kitaifa wanasema.

Maafisa wa uokozi kutoka Brazil wamewaokoa watu 350 kutoka sehemu zilizokabiliwa na mafuriko siku ya Jumapili.

Hapo jana Jumapili msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza masikitiko yake kutokana na kimbunga Kenneth.

Jimbo la Cabo Delgado halina watu wengi kama eneo lililoathirika na kimbunga Idai na inavyoonekana sehemu kubwa iko katika ardhi ya juu.

Hilo kwa pamoja na tahadhari za mapema kutoka kwa maafisa husika kabla ya kutokea kimbunga hicho huenda ikasaidia kuzuia hasara ikilinganishwa na wakati wa kimbunga Idai.

Lakini taarifa zinasema maelfu ya makaazi yameharibiwa kutokana na upepo mkali, na ene hilo limekabiliwa na mashambulio ya wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya kiislamu katika miezi ya hivi karibuni, jambo ambalo linaonekana huenda likatatiza utoaji wa msaada.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents