Habari

Hali ya joto kali Dar kuendelea mpaka Januari, TMA waeleza sababu

Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) imesema hali ya joto kali na jua vinavyoshuhudiwa katika Mikoa ya Ukanda wa Pwani vinatokana na uhafifu wa mvua za vuli ambazo hazijanyesha kwa kipindi cha miezi miwili tofauti na matarajio.

Meneja wa Kituo Kikuu Cha Utabiri, Samwel Mbuya amesema kwa sasa utabiri wao hauoneshi kama kutakuwa na mvua nyingi kutokana na jua kuwa katika usawa wa utosi.

“Joto limeongezeka kutokana na mwenendo wa kawaida wa jua la utosi na mtawanyiko hafifu wa mvua za vuli. Mvua zinaponyesha huwa zinapoza joto, tunatarajia hali hii itakwenda mpaka Januari,” amesema Mbuya.

Mbuya amesema hali hiyo ya juakali na joto vitaendelea hadi mwezi Januari mwakani huku matarajio yakionesha mwezi Februari huenda kukawa na juakali zaidi.

Meneja huyo amewataka wananchi waendelee kufuatilia utabiri wa hali ya hewa ili kufahamu mabadiliko yanayojitokeza mara kwa mara.

Kwa upande wa watalaamu wa masuala ya afya wanasema joto linapoongezeka huchangia kudhoofisha nguvu ya mwili katika utendaji wa kazi, hususan pale mtu anapokuwa sehemu ya wazi.

Wanasema, mara kwa mara mtu anapaswa kunywa maji mengi ikiwa ni njia mojawapo ya kuboresha ufanisi wa mifumo katika mwili wa binadamu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents