Uncategorized

Hapatoshi Mapinduzi Cup Yanga Vs Azam, rekodi inawabeba wana lamba lamba yenye Donald Ngoma na Chirwa

Michuano ya kombe la Mapinduzi inaedelea huko Visiwani Zanzibar ambapo mechi kubwa hii leo ni wana lamba lamba Azam FC itakayoshuka katika dimba la Amaan kumenyana na Yanga majira ya saa 2:15 usiku.

Mchezo unatarajiwa kuwa mkali na kuvutia hasa kutokana na vikosi vya timu zote mbili kuonekana kuwa imara kwenye ligi kuu ya Tanzania Bara ambapo sasa wana kutana kwenye michuano hiyo ya Mapinduzi Cup.

Mbali na ubora na uimara wa timu zote mbili lakini pia washambuliaji wawili ambao ni Donald Ngoma pamoja na Chirwa wakiwa chini ya kocha, Hans van Pluijm watawakabili waajiri wao wa zamani Yanga huku wakitaka kuwaonyesha kile walichonacho kwenye miguu yao.

Takwimu za kocha, Hansvan Pluijm aliyewahi kuifundisha miamba hiyo ya soka yenye maskani yake mitaa ya Jangwani inammbeba zaidi kwani tangu alipoondoka na kujiunga na Singida United amekutana nayo mara tatu na kufanikiwa kupata sare mbili ya 0 – 0 na 1 –1 kwenye michezo ya ligi na kuifunga kwa mikwaju ya penati katika mashindano ya FA Cup.

Lakini kwa upande wa nyota wake Donald Ngoma pamoja na Obrey Chirwa wao watakuwa wanakutana na Yanga kwa mara ya kwanza toka walipoachana na vigogo hao.

Lakini pia rekodi ya Yanga na Azam ni kwamba timu hizo zitakuwa zikikutana kwa mara ya nne kwenye michuano hiyo, mara tatu zilizopita Azam FC ikiwa na rekodi nzuri ya kupata matokeo dhidi ya Yanga, ikishinda mechi mbili na kutoka sare moja, ikiwa haijapoteza hata moja.

Mara ya kwanza zilikutana mwaka 2012 kwenye hatua ya makundi na Azam FC kuibuka kidedea kwa mabao 3-0, yaliyofungwa na gwiji wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’ kwa mkwaju wa penalti na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Kipre Tchetche, aliyefunga mawili.

Ushindi huo uliiwezesha Azam FC kutinga nusu fainali ya michuano hiyo na kukutana na Simba na kuiadhibu mabao 2-0, yaliyofungwa na Bocco na Gaudence Mwaikimba kabla ya kutinga fainali ikiichapa Jamhuri 3-1.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, walikutana na Yanga tena kwenye michuano hiyo mwaka 2016, kwenye mchezo wa hatua ya makundi ulioisha kwa sare ya bao 1-1, Azam FC ikifunga kupitia Tchetche kabla ya Yanga kusawazisha kupitia beki Vincent Bossou.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa mwaka juzi, kwenye hatua ya makundi, Azam FC ikipata ushindi mnono wa mabao 4-0, yaliyowekwa kimiani na Bocco, Joseph Mahundi, Yahaya Mohammed na Enock Atta.

Azam FC ikatinga nusu fainali na kuichapa Taifa Jang’ombe bao 1-0, lililofungwa na Frank Domayo ‘Chumvi’ kabla ya kutwaa taji la michuano ikiichapa Simba 1-0, Himid Mao ‘Ninja’ akiwa mfungaji wa bao hilo.


Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents