Michezo

Hat-trick dhidi ya Tanzania Prisons yampa kiburi Shaaban Idd aahidi kufanya makubwa

Mshambuliaji wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Shaaban Idd amesema kuwa kuuguza kwake majeraha kwa miezi saba nje ya uwanja kumemfanya kutokuwa na kasi kama aliyokuwa nayo msimu uliopita.

 

Usiku wa kuamkia leo, Shaaban ameiongoza Azam FC kuichapa Tanzania Prisons mabao 4-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wakati akifunga ‘hat-trick’ na kumfanya kufikisha jumla ya mabao nane msimu huu huku akiwa amekosa mechi za raundi ya kwanza nakuandika rekodi ya kufunga mabao sita ndani ya mechi nne zilizopita.

Mabao hayo nane yamemfanya kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita alipopandishwa timu kubwa akitokea Azam B, na kufunga mabao sita kwenye msimu wake wa kwanza wa ligi.

Alipozungumza na tovuti ya klabu hiyo, Shaaban amesema kuwa ili mlazimu kuvuta subira ili kurejea kwenye ubora wake na anamshukuru Mwenyezi Mungu hivi sasa ameanza kufanya vizuri huku akiahidi makubwa zaidi msimu ujao.

“Mimi sikuanza msimu kwenye raundi ya kwanza ila nimerudi raundi ya pili, nimekaa nje ya dimba zaidi ya miezi sita kwa hiyo nipate ile kasi yangu ambayo nilimaliza nayo msimu ulioisha ilibidi ichukue muda na lazima iwe hivyo kwa sababu mpira ni mchezo unaohitaji utulivu wa akili, utimamu wa mwili.

“Miezi sita si midogo kwa sababu sikuruhusiwa hata kugusa mpira, haikuwa na maana kwamba kiwango changu kimeshuka bali nilikuwa kwenye njia ya kunifanya mimi nifanye kazi kwa bidii ili kurejea katika kiwango ambacho nilikuwa nacho, namshukuru Mungu nimejitahidi na ndio kama unavyoona nimechanganya kwenye mechi za mwisho,” alisema.

Mabao sita, mechi nne

Mshambuliaji huyo ambaye mpaka sasa msimu huu ameshafunga mabao tisa kwenye mashindano yote, hakusita kuelezea furaha yake baada ya kuwa na muendeleza mzuri wa kufunga mabao, katika mechi nne zilizopita akiwa ametumbukia nyavuni mara sita.

“Ni rekodi nzuri pia mwenyewe nimeifurahia, kila mchezaji ambaye anapenda maendeleo yake na timu yake lazima acheze kwa rekodi inshallah Mungu akijalia naahidi kufanya kazi nzuri zaidi kwa ajili ya timu yangu,” alisema.

Shaaban amebakisha bao moja tu kufunga ili kufikia rekodi yake ya msimu uliopita, alipomaliza akiwa amefunga mabao 10 kwenye mashindano yote, sita kwenye ligi, moja Kombe la Mapinduzi na matatu Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) akimaliza nyuma ya aliyekuwa Nahodha wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor, aliyefunga 12 na kuwa kinara wa ufungaji ndani ya Azam FC.

Uvumilivu, sapoti kwa mashabiki 

Mshambuliaji huyo ambaye huitwa mara kwa mara kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ chini ya Kocha Mkuu, Salum Mayanga, aliwageukia mashabiki wa Azam FC na kuwaambia kuwa wawe na uvumilivu kwa wachezaji huku akiwataka waendelea kuisapoti timu.

“Mashabiki wawe na uvumilivu na wazidi kutusapoti kwa sababu hii ndio timu yao na sisi ndio wachezaji wao, kwenye shida na raha wazidi kuwa pamoja nasi,” alimalizia.

Mara baada ya mchezo wa jana, kikosi cha Azam FC kimefikisha jumla ya pointi 55 kikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo, kikiizidi Yanga pointi saba ambayo ina mechi mbili mkononi, huku Simba ikiwa tayari imeshatangaza ubingwa ikiwa nazo 68.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents